Fundisho moja kuu kabisa katika Biblia ni maarifa ya injili ya kweli. Unaelekea kujifunza ni kwa nini.
Elewa. Iko injili moja tu iliyo sahihi. Zingine zote ni upotoshaji, uliobuniwa na Shetani kuubadili ukweli wa Ujumbe wake wa ajabu. Ni ufahamu huu wa muhimu sana ambao mara nyingi watumishi wa Shetani huonekana kuupotosha kwanza.
Pale mwanzoni kabisa mwa huduma Yake, Kristo alifundisha, “Tubuni na kuiamini INJILI” (Marko 1:15). Lakini injili ya kweli ni nini? Je ziko zaidi ya moja ambazo Mungu anaziridhia? Majibu kwa hili na maswali mengine yanapatikana ndani ya Biblia—na kwa hakika ni MUHIMU kwako kuyaelewa. Lakini majibu yamebaki mafichoni kwa walio wengi sana.
Maarifa Mengi ya Uongo
Maelfu ya vitabu vipya vya kidini huchapishwa kila mwaka nchini Marekani! Vile vile kuna madhehebu na vikundi tofauti zaidi ya elfu mbili nchini Marekani! Ila, mkanganyiko na kutokukubaliana kuhusu majibu kwa maswali makuu ya maisha miongoni mwa wanaodai kuwa Wakristo, au katika ulimwengu mzima, umeongezeka zaidi kuliko wakati wowote. KWA NINI? Kwa nini yako maarifa mengi, na kwa wakati huo huo kuna ujinga mwingi juu ya ukweli kuhusu maswali MAKUU ya maisha?
Majibu yote kwa maswali haya yanahusiana moja kwa moja na INJILI!
Walio wengi wamefundishwa—na wanaamini—kwamba injili ni kuhusu Nafsi ya Yesu Kristo. Hakika, jukumu la Kristo ni somo la muhimu mno, lakini Yeye si injili. Biblia huonyesha kwamba jina la Yesu Kristo huhubiriwa sambamba na injili. Kwa mara nyingine, jukumu Lake ni la muhimu sana kwa Ukristo na ni lazima lieleweke, lakini Yeye si injili!
Baadhi hutangaza “injili ya wokovu” au “injili ya neema.” Wengine huamini “injili ya miujiza” au “injili ya ujamaa” au “injili ya vyakula” au “uponyaji” au “imani.” Bado wengine tu hufukiria “muziki wa injili” wanaposikia neno hili. Haya yote ni mawazo ya kibinadamu ambayo hupuuza ukweli wa Biblia!
Hebu turudi kwenye Marko 1, na tuangalie fungu la 14: “Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya UFALME WA MUNGU.” [injili ya ufalme wa Mungu] Hii ndiyo injili aliyohubiri Yesu. Na ni katika muktadha huo huo alisema, “Tubuni, na KUIAMINI INJILI.” Lakini, injili gani? Injili ya “ufalme wa Mungu.” Fungu la kwanza hurejelea ujumbe huu linaposema, “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo.” Injili ya Kristo ilikuwa juu ya UFALME WA MUNGU—si kitu kingine! Mtu awaye yote hana budi kuiamini injili hiyo, si bandia au mbadala. Ulimwengu kwa-njia-rahisi hauijui injili hii!
Wachache wanatambua. Lakini kwa nini? Kwa nini ni wachache sana leo-hii wanaoelewa vizuri mustakabali wa kustaajabisha wa mwito wa Kikristo? Paulo alivuviwa kufafanua: “Lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu” (1 Kor. 2:9-10). Pasipo Mungu kuifungua akili, haiwezekani kuelewa mambo ya Mungu. Vile vile haiwezekani hata kuja kwa Mungu (Yohana 6:44, 65). Kwa hakika, fungu hili linasema kwamba kusudi la Mungu halijawahi kuingia katika fikra za mwanadamu!
Mungu, kwa kusudi Lake la ajabu sana, amefunua ukweli wa injili kwa wachache sana kwa wakati huu—na amewaweka ndani ya Kanisa Lake. Walimwengu waliosalia wamepofushwa. Elewa hili! Ibilisi hataki wanadamu wafurahie kile ambacho yeye amenyimwa milele—uanakaya [kuwa memba] katika Familia ya Mungu, ambao utajifunza.
Wengi hawataamka dhidi ya udanganyifu—madanganyo kwa halaiki—wa “Ukristo” uliopotoshwa unaokataa kweli dhahiri za Biblia! Mpango wa Mungu kwa ajili ya wanadamu unaduwaza—usioweza kulinganishwa na chochote ambacho mwanadamu amekiunda kichukue mahali pake. Ulimwengu unapuuza maandiko yaliyo wazi, na dhahiri yapatikanayo kote katika Neno la Mungu kuhusu ufalme wa Mungu. Kitabu hiki kinafafanua ukweli wa kustaajabisha ambao wengi huupuuza—na kinafunua kile ambacho chaweza kuwa mustakabali wako!
Onyo Kali Kutoipotosha Injili
Somo hii ni la muhimu mno kiasi kwamba Mungu alimvuvia mtume Paulo kutoa onyo hili kwa Wagalatia kipindi kile na kwetu sasa: “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini, ijapokuwa sisi au malaika kutoka mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe” (1:6-9).
Hii ni kauli nzito sana! Baadaye kidogo, Paulo alisisitizia tumaini lake kwamba “kweli ya INJILI ikae pamoja nanyi” (2:5). Kwa hivyo iko injili moja ya kweli—na zingine zote za uongo. Sasa unaweza kuelewa vyema onyo la Paulo katika Wagalatia 5:7-9, lililorejelewa hapo awali.
Ingawa baadhi hudai kuwa Paulo alifundisha injili tofauti au injili ya nyongeza, ni wazi kwamba hakufanya hivyo. Kinyume na hilo, Mungu alimtumia Paulo kuonya dhidi ya kuruhusu fundisho la uongo kama hilo kwa kutangaza laana kwa mtu awaye yote, malaika au hata mtume yeyote—“Lakini, ijapokuwa sisi [akimaanisha, mitume]… atawahubiri ninyi injili nyingine yoyote”—anayechagua kukiuka amri hii (1:8)
Andiko zito kiasi gani—na ONYO!
Paulo alieleza kwamba mitume waliaminiwa na Mungu kuhifadhi injili ya kweli. Angalia 1 Wathesalonike 2:4: “Bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu.” Huo ni wajibu usioweza kuchukuliwa kirahisi. Watumishi wa kweli daima watafundisha kile ambacho Mungu ameamuru, si kile kinachowafurahisha wanadamu (ikiwa ni pamoja na “wasomi” wa Biblia). Hivyo, dai lolote kwamba Paulo alifundisha injili tofauti au ya pili (inayodhaniwa kuwa ni juu ya Kristo au ya “amani”) haiwezekani. Kwa hakika angekuwa anatangaza laana juu yake yeye mwenyewe!
Yesu Alitabiriwa Kuleta Injili
Yesu alikuja kama mtangazaji akibeba tangazo. Kila mahali alikoenda Alitoa tangazo hilo hilo kuhusu kuja kwa SERIKALI BORA itawalayo-ulimwengu itakayosimamishwa wakati wa Kurudi Kwake.
Alipokuwa akinena kwa kundi la wasikilizaji jangwani, Kristo alifafanua kusudi Lake—wajibu Wake. Angalia jinsi Alivyofafanua utume Wake: “Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya UFALME WA MUNGU katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa (Luka 4:43).
Mathayo anaangazia zaidi suala hili: “Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri HABARI NJEMA YA UFALME, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu” (Math. 4:23). Kazi ya Kristo ilikuwa ni kupeleka ujumbe wa ufalme wa Mungu katika miji yote ya Israeli. “Alitumwa” kwa kusudi hili.
Katika Agano la Kale, Yesu alitabiriwa kuja kama MJUMBE. Angalia Malaki 3:1: “Angalieni, namtuma mjumbe wangu [Yohana Mbatizaji], naye ataitengeneza njia mbele Yangu; naye Bwana, mnayemtafuta, atalijilia hekalu lake ghafla; naam, yule MJUMBE [Kristo] wa agano, mnayemfurahia.”
Kristo alikuwa “MJUMBE”, si ujumbe wenyewe. Ujumbe Wake kuhusu ufalme wa Mungu ndiyo kiini hasa—kitovu!—cha Biblia nzima.
Sasa linganisha aya katika Malaki na nyingine katika Agano Jipya: “Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana [maandiko ya Agano la Kale pekee ndiyo yaliyohubiriwa mpaka Yohana Mbatizaji]; tangu wakati huo habari njema ya UFALME WA MUNGU hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu” (Luka 16:16). Kumbuka kwamba, katika Marko, Kristo alihubiri “ufalme wa Mungu” na akauita injili.
Shetani, aliyejua kwamba Kristo alitabiriwa kuhubiri Ujumbe ambao anauchukia, kupitia Mfalme Herode, alitafuta Kumuua Akiwa angali mtoto mchanga. Hii ndiyo sababu ibilisi pia alitafuta kumjaribu kule nyikani (Math. 4:1-11). Alijua kuwa kama angefaulu katika jaribio moja wapo, basi angevuruga Mpango wa Mungu na kubaki na mamlaka juu ya mataifa ya ulimwengu. Pia tutajifunza zaidi juu ya hili baadaye.
Maana ya “Injili”
Neno “injili” ni neno la Kiingereza cha zamani lenye maana ya “god spell” yaani habari njema. Neno “ufalme” pia ni neno la Kiingereza cha zamani, lenye maana rahisi ya serikali. Tunaweza kusema kwa usahihi kwamba Kristo alihubiri “habari njema ya serikali ya Mungu.” Tutajifunza juu ya nani, nini, wapi, lini, kwa nini na ni vipi HABARI NJEMA hii inahusiana na unabii mkuu wa Biblia.
Neno injili linapatikana mara 101 katika Biblia. Wakati mwingine linapatikana pekee yake, na wakati mwingine “ya ufalme” hulifuatia. Wakati mwingine hujumuisha “ya ufalme wa Mungu” au usemi unaolingana na huo “ya ufalme wa mbinguni.” Angalia kwamba inasema, “wa mbinguni,” siyo “huko mbinguni.” Ni ufalme wa mbinguni na kuna tofauti kubwa. Kama ilivyo kwamba ufalme wa Mungu, si ufalme katika Mungu, vivyo hivyo ni kweli kuhusu ufalme wa mbinguni au ufalme wa mbingu. Hili ni jambo muhimu kulielewa.
Kote katika Agano Jipya, neno “ufalme” hupatikana mara 27, “ufalme wa Mungu” mara 75 na “ufalme wa mbinguni” mara 34. Ni wazi kwamba yote haya ni kitu kimoja na yanafanana.
Sasa elewa jambo hili. Somo la ufalme wa Mungu si tu kwamba ni mada kuu katika Agano Jipya, lakini pia ndio mada kuu katika Biblia NZIMA. Bado, ajabu ni kwamba, wengi wanaelewa kidogo au hawajui kabisa habari zake. Watumishi wa makanisa ya ulimwengu huu hawaijui injili ya kweli na kamwe hawahubiri juu yake. Kwa hivyo, karibu ulimwengu mzima unasimama katika ujinga kamili kuhusu moja ya ukweli mkuu katika Neno la Mungu. Ni ajabu, lakini ni kweli!
Pia, wale WOTE ambao wakati mmoja walijifunza ukweli huu lazima wawe makini wakati wote, usije ukawaponyoka (Ebr. 2:1).
Mitume Walihubiri Injili ya Kweli
Kuna ushahidi gani kwamba waandishi wengine wa Agano Jipya walihubiri ujumbe huu huu? Ni mwingi sana!
Petro alihubiri ufalme. Angalia: “Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika UFALME wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo” (2 Pet. 1:11).
Ndivyo alivyofanya mtume Yakobo: “Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa UFALME aliowaahidia wampendao?” (2:5).
Maelezo ya Mathayo hutaja usemi “injili ya ufalme” mara tatu tofauti. Huu hapa ni mfano mwingine ambao ni karibu sawa na 4:23, iliyokwisha kunukuliwa: “Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri HABARI NJEMA YA UFALME, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina” (9:35).
Katika mingi ya mifano Yake, Kristo alifundisha mambo ya msingi ya ufalme wa Mungu. Mathayo peke yake, hasa kwa njia ya mifano, hufanya rejea zaidi ya hamsini kwa ufalme wa Mungu unaokuja.
Luka ameandika kuwa Yesu Kristo aliwaagiza wanafunzi wake kuhubiri ujumbe huu huu: “Akawaita wale Thenashara...Akawatuma wautangaze UFALME WA MUNGU” (9:1-2). Muda mfupi baadaye, aliwatuma wengine sabini waende kuhubiri, nao pia walibeba ujumbe wa “UFALME WA MUNGU” (10:1, 9).
Yohana ameyaandika maneno ya Kristo mbele ya Pontio Pilato usiku ule aliposalitiwa. Hiki ni kiashiria muhimu kukielewa. Kristo alisema, “UFALME Wangu si wa ulimwengu huu [jamii hii ya sasa]” (Yohana 18:36). Baadaye tutagundua undani wa jinsi ambavyo serikali ya Mungu itasimamishwa duniani.
Kumbuka kwamba Filipo, shemasi, alihubiri ufalme kwa Wasamaria (Matendo 8:12).
Tambua kwamba katika kuhubiri alitenganisha ufalme na Kristo: “Lakini walipomwamini Filipo…kuhusu ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.”
Filipo hakuhubiri injili ya ufalme pekee, lakini pia aliitofautisha na fundisho juu ya Yesu Kristo. Tumia muda kusoma habari hii yote. Kumbuka mjumbe sio ujumbe. Kristo si injili. Hata hivyo, Husimama kando yake moja kwa moja na atatawala dunia nzima wakati ufalme utakaposimamishwa.
Hivyo basi Luka, mwandishi wa Matendo, hutofautisha zaidi kati ya kuhubiri juu ya ufalme wa Mungu na kuhubiri juu ya Yesu Kristo! Wakati yote ni ya muhimu sana, ni wazi kwamba ni masomo mawili tofauti!
Tumetatua tatizo ambalo baadhi ya watu hudai kwamba Paulo alihubiri “injili tofauti.” Kwa hakika hawa hawana habari kwamba ni Paulo ambaye Mungu alimtumia kutangaza laana kwa yeyote aliyefanya hivyo (Gal. 1:8-9). Tumeona kwamba Paulo alihubiri ufalme wa Mungu. Hata hivyo, utaona mafungu mawili katika Matendo, ambayo huonyesha kwamba hakupuuzia somo la pili juu ya jukumu la Kristo katika mchakato wa wokovu.
Kwanza, hebu tuthibitishe kwamba Paulo alihubiri ufalme wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Matendo 19:8 husema: “Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya UFALME WA MUNGU.” Yako maeneo mengi katika nyaraka zake ambapo Paulo alifundisha ufalme kwa makanisa mbalimbali ya watu wa Mataifa. Ujumbe wake ulikuwa huo huo wakati wote, akiendelea kuhubiri na kurejelea ufalme wa Mungu.
Chunguza hili kutoka Matendo 20:25: “Niliowahubiria UFALME WA MUNGU…wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo” (fu. 21). Maelezo haya yanaweka wazi kwamba Paulo alihubiri injili hiyo hiyo—pia sambamba na jukumu la Kristo—kwa Wayahudi na watu wa Mataifa. (Kimsingi Waefeso walikuwa waongofu kutoka kwa watu wa Mataifa.)
Kisha, angalia sura ya 28:30-31: “Na Paulo akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za UFALME WA MUNGU, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo.” Kama Filipo, Paulo alielewa kuwa injili na Yesu Kristo alikuwa ni nani, yalikuwa ni masomo mawili tofauti.
Mwisho, angalia aya moja zaidi mahali ambapo Paulo alibainisha tofauti kati ya injili na Nafsi ya Kristo, kwa kurejelea tena kwa ufupi 2 Wakorintho 11:4: “Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri… au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye” (maelezo ya pembeni kwa usahihi hutamka usemi wa mwisho “na mimi”). Paulo aliwahimiza Wakorintho kuwakataa waalimu wa uongo na kushikilia kile alichokuwa amewafundisha. Kwa wazi alitofautisha mafundisho ya Yesu wa uongo na injili ya uongo kama makosa mawili tofauti.
Jiulize mwenyewe tena: Kama Kristo ni injili, basi kwa nini Paulo (mara nne) na Filipo huyaongelea kama mambo mawili tofauti?
Kila Nabii wa Agano la Kale Alihubiri Ufalme
Wengi wamedhani kwamba injili ni ujumbe wa Agano Jipya peke yake. Hakuna kitu ambacho kinaweza kuwa mbali na ukweli kama hiki! Kwa hakika Biblia imejaa maeneo, katika Agano la Kale na Jipya, yanayoelezea vipengele mbalimbali na unabii kuhusu ufalme wa Mungu.
Hebu tuchunguze kauli ya kushangaza ya Petro inayopatikana katika Matendo 3:19-21: “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.”
Angalia kwamba Petro anarejelea Kuja kwa Kristo—“kuwako kwake Bwana” (fu. 19), na fungu la 20 likisema kwamba Mungu “apate kumtuma Kristo Yesu.” Fungu la 21 huelezea ufalme wa Mungu kama “kufanywa upya vitu vyote.” Petro alitamka kwamba huku “kufanywa upya” (Kristo akisimamisha ufalme Wake) ni zamani ambazo “zilinenwa na Mungu kwa… manabii Wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.”
Hii ni kauli ya kushangaza! Lakini je, ni kweli?
Inawezekana kweli Mungu alimtumia kila mmoja wa manabii wake kutangaza ufalme Wake? Kwa nini wasomi wa Biblia na watu wa dini hupuuzia hili—au hata kulikataa hapo hapo? Hebu tuchunguze Agano la Kale.
Wahubiri-Kabla ya Gharika
Yuda aliandika, “Na Henoko [Babu-mkuu wa Nuhu]…alitoa maneno ya unabii…akise- ma, Angalia Bwana YUAJA… ili afanye hukumu juu ya watu WOTE” (fu. 14-15). Ni wazi hii humrejelea Yesu Kristo akirudi kusimamisha serikali, inayoyatawala mataifa YOTE.
Katika 2 Petro 2:5, Nuhu hurejelewa kuwa “mhubiri wa haki wa nane”. Yuda aliandika kuwa Henoko alikuwa wa “saba kutoka Adamu.” Hivyo, Nuhu aliyemfuatia, anarejelewa kuwa wa “nane.” Ukianza na Habili, ukimjumlisha na Henoko, kulikuwa na wanaume saba ambao walibeba jukumu hili hapo nyuma kabla ya Nuhu. Maisha ya wanaume hawa wanane yalienea kipindi chote kati ya Adamu na Gharika na wote walihubiri ujumbe huo huo.
Uchunguzi makini wa Yuda hufunua kuwa Henoko alihubiri kuhusu dhambi na haki. Wakati mengi yanaweza kusemwa kuhusu kipindi hiki cha karne kumi-na-sita-na-nusu, inatosha kusema, watu hawa wote walizungumzia ujumbe ule ule. Kumbuka Petro alisema, “…tokea mwanzo wa ulimwengu.”
Nani mwingine alihubiri ufalme wa Mungu?
Ibrahimu, Musa, Samweli na Daudi
Je, kuna ushahidi kwamba injili ilihubiriwa katika kipindi kilichofuata baada ya Gharika?
Katika Mwanzo 12:3, Mungu alimwambia Ibrahimu, “Katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.” Fungu hili pia limerejelewa kwenye Wagalatia 3:8, lakini limesemwa tofauti kidogo: “…katika wewe [Ibrahimu] mataifa yote watabarikiwa.” Fungu hili hili husema kwamba injili “ilihubiriwa zamani kwa Ibrahimu.”
Hii inavutia! Si tu kwamba Ibrahimu alihubiriwa injili (bila shaka na Melkizedeki—Kristo), lakini pia ilihubiriwa katika Mwanzo, kupitia maandiko ya Musa, kuhusu Ibrahimu! Sasa fikiri. Inawezekanaje mataifa yote ya dunia kubarikiwa isipokuwa Kristo atakuwa amesimamisha serikali Yake duniani?
Ingawa Musa hakuwa “mhubiri wa haki” au mtume, alikuwa nabii na mwamuzi, na mtu wa kwanza ambaye Mungu alimwinua kuwaongoza Israeli. Pengine hukuwahi kumfikiria Musa kama mmoja wa waliohubiri injili. Bado, Biblia hufunua kwamba alihubiri, kwa Israeli wa zamani, walipokuwa jangwani. Tuliona kwamba Mwanzo 12:3, hurejelea injili, kama ilivyo Hesabu 24:17-19, na mafungu haya yote yaliandikwa na Musa.
Matendo 3:22 kwa wazi husema Musa alitangulia kunena kwamba Mungu atamwinua Yesu Kristo kama Nabii mkuu (Torati 18:15) kuhubiri kwa ulimwengu mzima (Matendo 3:23) wakati wa Kurudi Kwake! Wengi wanaelewa tu juu ya Musa kuwaongoza Israeli kutoka Misri, na hawajui kabisa jinsi Mungu alivyomtumia katika njia hii.
Waebrania 3:9 na 4:2 pia huonyesha kwamba Musa alihubiri injili kwa Israeli wa zamani. “Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao [Israeli wa zamani]” (4:2). Mafungu haya, pamoja na Matendo 3, huonyesha kwamba hii ilijumuisha kipindi chote mpaka—na cha—Samweli!
Matendo 3:24 humrejelea Samweli pia kama aliyehubiri injili. Angalia: “Naam, na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena [ikimaanisha kila mmoja], walihubiri habari za siku hizi [Kuja kwa Kristo na ufalme wa Mungu].” Hizi ni kauli nzito na za wazi. Haziwezi kufunikwa. Jiwezeshe mwenyewe kutumia muda kutafakari juu ya kile ulichokisoma. Fungu hili linatamka, “manabii WOTE wa Mungu…wote walionena…walihubiri habari za siku hizi.”
Hatimaye, ingawa kila mtu anajua kuwa Daudi alikuwa mfalme, karibu hakuna anayefahamu kwamba alihubiri ufalme wa Mungu. Katika Zaburi 67:4, aliandika, “… Maana kwa haki Wewe [Bwana] utawahukumu watu, na kuwaongoza mataifa walioko duniani.” Kauli hii ni kielelezo dhahiri kwa serikali ya Mungu inayokuja.
Isaya, Yeremia, Ezekieli na Danieli
Nabii Isaya alitoa kauli za wazi kabisa kuhusu ufalme wa Mungu, kuhusu vile utakavyotokea na kuleta amani kwa mataifa yote duniani. Vile vile aliweka wazi kwamba ufalme wa Mungu huhusisha SERIKALI. Angalia “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na UWEZA WA KIFALME utakuwa begani mwake; Naye ataitwa Jina Lake, Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani. Maongeo ya ENZI Yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na UFALME wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza; Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele” (9:6-7).
Unabii huu uko wazi mno kiasi kwamba hauhitaji ufafanuzi zaidi!
Nabii Yeremia alitangulia kusema, “Tazama siku zinakuja, asema BWANA, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la Haki [Kristo]; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA NI HAKI YETU”(23:5-6; pia soma fu. 7-8).
Kama ilivyo kwa Isaya, mafungu haya hayahitaji ufafanuzi zaidi. Yeremia anatoa maelezo ya wazi ya matukio ambayo yanaweza kuelezewa tu kama kipindi baada ya ufalme wa Mungu kuwa umekwisha kuja duniani. Hivyo, alihubiri injili kwa Nyumba ya Yuda.
Kitabu cha Ezekieli huelezea wakati ambapo Mungu atawakusanya watu Wake kutoka matekani watakakochukuliwa siku zijazo. Hiki ni kipindi kinachofuata mara tu baada ya Dhiki Kuu (Math. 24:21-22)—kipindi cha maafa kwa wazao wa leo wa Israeli wa zamani. Sasa angalia: “Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe” (36:24).
Mafungu kumi yanayofuata huelezea kipindi cha ujenzi mpya na mafanikio ambayo yanaweza kutokea tu baada ya Kurudi kwa Kristo. Chukua muda uyasome.
Danieli aliandika hivi: “Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha UFALME ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa ENZI yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele” (2:44).
Je, nabii huyu alihubiri ufalme wa Mungu? Biblia hujibu ndiyo—na tutakuja kuona baadaye kuwa alifanya hivyo katika maeneo mengine mengi!
Manabii Wadogo Wote
Inaweza kuonyeshwa kwamba, kwa njia moja au nyingine, wale wote ambao hujulikana kama “Manabii Wadogo” walihubiri injili ya ufalme wa Mungu (inawezekana kuacha Yona.) Kumbuka, kuuona usemi “injili ya ufalme wa Mungu” si njia pekee ya kuielezea injili! Mafungu ya Mwanzo 12:3 na Wagalatia 3:8 yamekwisha kudhihirisha hili.
Yapitie tena mafungu yafuatayo. Katika kila fungu, utaona kuwa yanarejelea ufalme wa Mungu, moja kwa moja au kwa namna nyingine: Hosea 2:16, 19; 3:5; Yoeli 2:21-27; Amosi 9:11-15; Obadia 21; Mika 4:1-3; Habakuki 2:14; Zefania 3:14-20; Zakaria 14:1-3, 8-9; Malaki 3:1-3.
Baada ya kusoma maandiko haya, ni wazi kwamba Petro alikuwa sahihi, na kwamba “...zije zamani za kufanywa [urejeshaji] upya vitu vyote zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu,” ambazo zaweza kutokea tu pale serikali ya Mungu itakapokuja duniani.
Ni muhimu sana kusema jambo moja la mwisho. Matendo 3:21 husema, “Mungu amenena kwa kinywa cha…” Injili ya ufalme ni ujumbe kutoka kwa Mungu.
Lazima iwe wazi kwamba ni MUNGU anayenena kupitia kwa aina yoyote ya mtumishi Anayemtumia—nabii, mzee, mwamuzi, shemasi, mhubiri wa haki, mfalme, mchungaji, mwinjilisti au mtume! Kama kweli mtu alikuwa mtumishi wake, wakati wote Mungu alinena ujumbe huu huu kupitia kwake—“tokea mwanzo wa ulimwengu”!
Je, Kuna Injili Iliyojitenga ya Yesu Kristo?
Kama ilivyotajwa, Marko 1:1 huzungumzia “Mwanzo wa injili ya Yesu Kristo.” Hebu tuulize: Je, “injili ya Yesu Kristo” ni tofauti—injili—ya pili? Je, Paulo alisahau kwamba kulikuwa na injili nyingine kando ya ile inayohusu ufalme?
Jibu ni “Hapana” ya msisitizo! Lakini wahubiri wengi hufundisha kwamba injili ya Yesu Kristo ni kuhusu Kristo, pia wakidai kwamba Yeye ndiye ufalme wa Mungu na kwamba injili ya ufalme ni Kristo. Tumekwisha kuona kwamba huu ni uongo, na hautokani na Biblia kabisa! Injili ya Yesu Kristo ni injili Yake—ujumbe Wake kuhusu ufalme wa Mungu!
Tumeona kwamba Yesu alikuwa Mjumbe aliyetumwa kutoka kwa Mungu akiwa na TANGAZO! Haikuwa kuhusu Yeye Mwenyewe—ilihusu ufalme wa Mungu ukija kutawala juu ya dunia yote. Katika Yohana 12:49-50, Yesu alisema, “Kwa sababu Mimi sikunena kwa nafsi Yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, Yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo Lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo Mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.” Lazima iwe wazi sasa kwamba Kristo alitenda kama mjumbe—kama MSEMAJI kwa ajili ya ufalme wa Mungu.
Katika Yohana 14:24, Yesu alisema, “nalo neno mnalolisikia silo Langu, ila ni Lake Baba aliyenipeleka.” Kristo alileta ujumbe wa Baba—sio Wake mwenyewe. Jambo hili sasa lazima liwe limekuwa wazi kabisa. Kumbuka, alisema katika Luka 16:16 kwamba “Torati na manabii vilikuwapo [hubiriwa] mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa.”
Hicho ndicho Kazi hii inafanya leo. Kupitia kitabu hiki, na vingine vingi, ukweli wa ufalme wa Mungu unahubiriwa kwako na kwa mamilioni wengine.
Ufalme wa Mungu Unakuja
Usifanye kosa lolote! Wakati hali ya ulimwengu inakaribia migogoro ya mwisho, hakuna mwanadamu aliyeweza kuleta serikali moja yenye kutawala dunia nzima ambayo ingeweza kufanikiwa. Yesu Kristo atarudi hivi karibuni na kusimamisha ufalme WAKE.
Wanafunzi hawakuelewa ni lini Kristo angesimamisha serikali ya Mungu duniani. Ilimlazimu kuwaeleza kwa kutumia mfano. Angalia: “Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa UFALME WA MUNGU utaonekana mara” (Luka 19:11). Mfano huu mrefu hufafanua kwamba muda mrefu ungepita kabla ufalme haujaja.
Kabla ya kupaa Kwake mbinguni, katika Matendo 1, baada ya kukutana mara kadhaa na wanafunzi Wake, Kristo alikutana nao mara moja na ya mwisho. Mpaka mwisho kabisa, Aliendelea kuwafafanulia zaidi ufalme wa Mungu. Lakini walibaki wamekanganyikiwa kuhusu ni lini utasimamishwa: “hata siku ile alipochukuliwa juu... [alikuwa] akiyanena mambo yaliyouhusu UFALME WA MUNGU… Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli UFALME?” (fu. 2-3, 6).
Kristo alifafanua, “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira…” (fu. 7). Hata leo hatuwezi kujua hasa ni lini utakuja, lakini tunaweza kujua kuwa uko karibu.
Sasa angalia Danieli 7:18: “Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele.” Kisha fungu la 22 husema, “Hata akaja huyo Mzee wa Siku [hapa ni Kristo, na Baba ametajwa kwenye fungu la 13], nao watakatifu Wake Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme.”
Mwisho, angalia fungu la 27: “Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu Wake Aliye Juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka [watawala] watamtumikia na kumtii.”
Danieli alijua kwamba siku moja watakatifu watatawala na Kristo duniani!
Hubiri la kwanza la Yesu lililoandikwa, huitwa “Hubiri juu ya Mlima,” husema kwamba “wapole watairithi nchi” (Math. 5:5). Kwa hakika, Kristo alikuwa anamnukuu Daudi, aliyeandika ripoti hii katika Zaburi 37:11—ni mahali pengine Daudi alipoitangaza injili. Maneno yaliyotumika hapo ni yale yale. Unabii mwingine pia huonyesha kwamba siku moja Daudi mwenyewe atatawala juu ya makabila yote ya Israeli (ona Ezekieli 34) ndani ya ufalme wa Mungu.
Angalia mafungu matatu tofauti katika Ufunuo. Kristo amenukuliwa kupitia Yohana akisema, “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja Nami katika kiti Changu cha enzi, kama Mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba Yangu katika kiti Chake cha enzi” (3:21). Pia 2:26-27: “Na yeye ashindaye…nitampa mamlaka juu ya mataifa: naye atawachunga kwa fimbo ya chuma.” Mwisho, “ukawafanya kuwa UFALME na MAKUHANI kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi” (5:10).
Je, dini yoyote iliyoundwa imekuambia kuhusu mojawapo ya mafungu haya? Bila shaka hakuna kabisa. Japokuwa yamekuwepo ndani ya Biblia kwa maelfu ya miaka.
Si ajabu kwamba Kristo alipokuwa akishtakiwa kwa ajili ya maisha Yake, Aliongeza zaidi kwenye ripoti Yake iliyonukuliwa mapema katika kitabu, “UFALME Wangu sio wa ulimwengu huu. Kama UFALME Wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi Wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi: Lakini UFALME Wangu si wa kutoka hapa” (Yohana 18:36). Katika majibizano haya, Pilato alikuwa amemuuliza, “Wewe u mfalme basi?” Kristo alijibu, “Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya Mimi nalikuja ulimwenguni…” (fu. 37).
Yesu alielewa kikamilifu kwamba Alizaliwa kuwa Mfalme!
Kristo Kuwa Mfalme
Kuja kwa Kristo Mara ya Kwanza lilipaswa kuwa tukio kubwa. Isaya alitabiri kuzaliwa Kwake na bikira: “Kwa hiyo BWANA Mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto Mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli” (7:14).
Kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, malaika alimtokea Mariamu kumfafanulia kusudi la Mungu na kile kilichokuwa kinaenda kumtokea: “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina Lake Nazareti, kwa mwanamwali… Mariamu” (Luka 1:26-27).
Kuanzia fungu la 30, Gabrieli anaelezea zaidi kuhusu Kristo na jinsi ambavyo hatimaye atatawala kwenye kiti cha enzi cha Daudi. Angalia: “Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto Mwanamume; na jina Lake utamwita YESU. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye Juu, na Bwana Mungu atampa KITI CHA ENZI cha Daudi, baba Yake. ATAIMILIKI nyumba ya Yakobo hata milele, na UFALME Wake utakuwa hauna mwisho” (fu. 30-33).
Kristo kamwe hakuwa na shaka kuhusu utume na kusudi la maisha Yake. Hii ndiyo sababu alifululiza kuhubiri ufalme wa Mungu popote alipokwenda.
Isaya aliongea kwa undani zaidi kuhusu jinsi ambavyo ufalme wa Mungu utaenea duniani, hatimaye kufunika mataifa yote: “Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia Zake, nasi tutakwenda katika mapito Yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe” (2:2-4).
Unabii ulio sawa na huu umerudiwa kwa msisitizo katika Mika 4:1-3. Aya hizi hutabiri kwamba ufalme wa Mungu utaenea ulimwenguni. Hii ndiyo sababu mfano mmoja wa Kristo ulilinganisha ufalme na chachu (Luka 13:20-21), ambayo daima husambaa na kujaa ilimowekwa. Kusudi kuu la maisha yako ni kushiriki kuieneza SERIKALI ya Mungu kwa wakati ujao.
Mbele ya jengo la Umoja wa Mataifa kuna sanamu ya mtu mkubwa akifua panga kuwa jembe. Nimeiona mara nyingi sana, kwa sababu niliendesha huduma za kanisa mtaani hapo mkabala na mahali ilipo kwa miaka kadhaa. Lakini hakuna mtu anayeonekana kutilia maanani tena, au hata kuamini, unabii wa kushangaza unaoelezewa na sanamu hili maarufu.
Yesu Kristo alikuja kuwa MFALME ambaye siku moja ATATAWALA duniani. Atakaporudi, mateso, masikitiko, huzuni na matatizo yote ya dunia na maovu vitatoweka—na amani ya dunia “itajitokeza,” halisi sambamba na furaha kuu, mapatano na mafanikio tele kwa mataifa yote. Hakuna serikali ya mwanadamu iliyoweza kuleta mambo haya hata kwa nchi moja duniani. Hiki ndicho kiini cha injili ambayo Kristo aliileta.
Je, unaiamini? Utaiamini?
Bado Ufalme wa Mungu Lazima Uhubiriwe Leo
Katika unabii wa Mlima wa Mizeituni kwenye Mathayo 24 (na 25), Kristo aliulizwa kuhusu matukio ambayo yangekuwa ishara ya Kuja Kwake Mara ya Pili na mwisho wa ulimwengu (zama). Alijibu kwamba matukio na hali mbalimbali tofauti vitatokea kwanza.
Tukio moja linalotangulia Kurudi kwa Kristo limeelezewa katika fungu la 14: “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.” Injili ya kweli ilitabiriwa kuhubiriwa mpaka “mwisho utakapokuja.” Hii inamaanisha wazi kwamba mtu fulani atakuwa anaihubiri sasa, katika zama yetu, kwa sababu mwisho bado haujaja.
Historia kidogo: Maarifa ya injili ya kweli yalirejeshwa na Herbert W. Armstrong (1892-1986). Injili ilikuwa haijahubiriwa kwa ulimwengu kwa takribani karne 19 mpaka bwana Armstrong alipoanza kuihubiri mwezi Januari 1934, wakati unabii wa Mathayo 24:14 ulipoanza kufunuliwa. Elewa! Tangu karne ya kwanza ulimwengu wote haukuwahi kusikia ujumbe huu. Kwa kipindi chote cha huduma ya miaka 52, mpaka kifo chake mwaka 1986, Mungu alimtumia bwana Armstrong kuwafikishia ufahamu huu mamia ya mamilioni. Huyu ndiye mtu aliyenifundisha mimi injili ya kweli na ambaye chini yake nilifunzwa kuweza kuupeleka ujumbe huu huu kwa ulimwengu.
Kumbuka, mwisho bado haujaja. Kwa hiyo, Kanisa la Mungu Rejeshwa linaendeleza utume huu, kwa ujasiri likihubiri ukweli huu mkuu kati ya kweli za kiunabii. Kuwasili kwa ufalme wa Mungu ni hakika—hakuna shaka! Utakapofika, wewe pia unaweza kuwa sehemu yake.
Mpango wa Miaka-7,000
Ukiwa umetengwa na Mungu kwa sababu ya dhambi (Isa. 59:1-2), ubinadamu umeamini uongo wa mungu wa dunia hii kwa miaka 6,000. Muhula wa Mpango wa Mungu kwa wanadamu utachukua miaka 7,000. Wachache wameelewa hili. Wengi wameelewa kwa usahihi angalau mafungu machache yanayoelezea Utawala wa Kristo wa miaka 1,000 unaokuja, utakaoanza wakati wa Kurudi Kwake (Ufu. 20:4-6). Lakini hawajui chochote kuhusu Mungu kutenga miaka 6,000, au siku-milenia sita za “juma la siku-saba,” kwa ajili ya utawala wa mwanadamu, chini ya Shetani, kabla ya miaka 1000 ya “siku” ya saba. Tuko karibu sana na mwisho wa “siku ya sita.”
Hebu tuelewe! Biblia inasema, “Lakini, wapenzi, MSILISAHAU neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja” (2 Pet. 3:8; Zab. 90:4). Kwa hakika, wengi “wamepuuza” karibu KILA KITU ambacho Biblia hufundisha.
Lakini unaweza kujua!
Mwanadamu (chini ya utawala wa Shetani usioonekana) amepewa “siku” sita, au miaka 6,000, kujaribu njia zake, serikali, dini, falsafa, mifumo ya maadili na mitindo ya elimu. Chini ya ushawishi wa Shetani, ametenda dhambi na uasi kwa maagizo ya Mungu kipindi hiki chote. Na ameshajaribu kutibu athari zote mbaya zilizojitokeza, badala ya chanzo, ambacho ni uvunjaji wa amri za Mungu. Mungu anauruhusu ubinadamu kujifunza masomo magumu, machungu. Walio wengi ambao kamwe hawakuwahi kujua thamani ya ukweli wa Mungu, lazima wajifunze kwamba njia zao wenyewe hazifai kitu!
Muda mfupi ujao, ulimwengu utashuhudia kutimia kwa Ufunuo 11:15: “Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo Wake, Naye atamiliki hata milele na milele.”
Yesu Kristo alizaliwa kuwa Mfalme ambaye atatawala mataifa yote ya dunia milele akisaidiwa na wafalme wengine walio roho: “Na upanga mkali hutoka kinywani Mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma… ana jina limeandikwa katika vazi Lake na paja Lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA” (Ufu. 19:15-16).
Je, kuna mtu yeyote aliyewahi kukuambia juu ya aya hizi? Sikuwahi kujifunza habari zake au hata kuzisikia katika kanisa la ujana wangu—na bado, ndizo hizi hapa, zimeandikwa kwa maana ya wazi bila utata kwa wote watakaotii.
Ufalme wa Mungu Wafafanuliwa
Mathayo 6:33 inasema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki Yake…”
Kama unatafuta kitu fulani kwanza katika maisha, ingekuwa vyema ukaelewa ni nini hasa unachotafuta.
Lengo kuu katika sura hii si kufafanua kwa undani ufalme wa Mungu. (Hii itafanyika baadaye). Ni kufafanua fasili ya injili ya kweli na uwezekano wa kustaajabisha wa ubinadamu.
Hivyo hebu tuelewe. Neno “ufalme” kwa urahisi humaanisha serikali. Kwa hakika, huwezi kuwa na serikali bila taifa la kutawala. Kwa hivyo, ufalme kwa uchache ni taifa moja pamoja na serkali yake.
Kuna vipengele vinne vya muhimu kwa ufalme wowote: (1) Ardhi, mali au eneo—liwe kubwa ama dogo. Kwa maneno mengine, ni lazima pawepo na mipaka halisi inayotambulisha eneo la ufalme; (2) mtawala, mfalme, mtawala mkuu au gavana anayeongoza serikali, (3) watu au wananchi wanaoishi katika eneo la utawala, na (4) mfumo wa sheria na kanuni sambamba na muundo msingi wa serikali. Hakuna ufalme uliokamilika bila kuwa na mambo haya yote ya msingi.
Lakini mambo haya yanahusika vipi na ufalme wa Mungu? Wengi hawajui mambo ya msingi ya ufalme wa Mungu. Je ni ufalme halisi wenye mahali halisi duniani, wenye watu na sheria, zikisimamiwa na mtawala? Wengi huamini ufalme ni kitu fulani kilichomo katika mioyo ya watu. Wengine wanaamini kuwa uko mahali popote utakapoona kanisa fulani. Bado wengine wanaamini kwamba ni Yesu Kristo mwenyewe. Baadhi wanaamini kwamba uko hapa duniani sasa na wengine wanaamini kwamba haujaja bado, lakini hawaelewi—hawana wazo—jinsi utakavyotokea.
Tunaweza kuuliza: Jinsi gani mtu anauingia ufalme wa Mungu?
Ni Lazima Mtu azaliwe Mara ya Pili Kuuingia Ufalme
Paulo aliandika kwamba Kristo ni “mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu” (Kol. 1:18), na pia “mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi” (Rum. 8:29). Yakiunganishwa, mafungu haya yanaonyesha kwamba Yesu ni mzaliwa wa kwanza tu kutoka kwa wafu, na wengine wengi watafuatia. Lakini ni lini, na katika nini, hawa wengine watazaliwa?
Katika Yohana 3:3, Kristo alimwambia Nikodemo, “Amin, amin [hii humanisha kweli, kweli], nakuambia, Mtu ASIPOZALIWA MARA YA PILI, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.” Katika fungu la 6, Kristo anaendelea, “Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.” Kwa urahisi tu amini maana dhahiri ya fungu hili. Ni lazima mtu afanyike roho ili KUUONA ufalme wa Mungu.
Paulo alifundisha, “nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu” (1 Kor. 15:50). Mafungu mawili yanayofuata hufafanua kuwa ufufuo utatokea wakati wa Parapanda ya Saba (mwisho), wakati “wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.”
Kristo atarudi wakati Parapanda ya Saba ya Ufunuo 11 italia. Huu ndio wakati ambao ufufuo wa wafu utatokea. Usilielewe vibaya tukio hili la upeo wa juu kabisa, litakaloelezwa kwa uangalifu zaidi baadaye. Inatosha kusema hapa, watu ambao hapo kabla walikuwa wanadamu wa nyama watabadilishwa kuwa roho—watazaliwa mara ya pili—na kuingia katika ufalme wa Mungu. Hakuna watu halisi wanaoweza kuuingia ufalme.
Yohana 4:24 inasema, “Mungu ni Roho.” Chini ya Baba, Kristo anaongoza ufalme Wake, ambao unaundwa na viumbe roho. Wakati wa Kurudi Kwake Kristo, kama mwanakaya [memba] wa Familia ya Mungu, atakuwa na wadogo wengi “ndugu wakiume na wakike,” watakaokuwa wamefuzu kutawala pamoja Naye.
Fikiria namna hii: Uko ufalme wa mimea, ufalme wa wanyama, falme za wanadamu na ufalme wa malaika. Vile vile kuna ufalme wa Mungu.
Sasa angalia Mwanzo 1:26: “Na tumfanye mtu kwa mfano WETU, kwa sura YETU.” Wakijirejelea wao wenyewe, Yule anayeongea anasema, “Sisi,” “Wetu” na “Yetu.” Huu ni uthibitisho kwamba katika Uungu wako zaidi ya mmoja—kwa sasa wako wawili! Katika andiko hili, neno la Kiebrania kwa ajili ya Mungu ni Elohim. Neno hili ni la wingi katika umoja kama kundi, timu, kamati au familia. Maneno haya yote yanawakilisha kitu kimoja, chenye washiriki kadhaa au watu.
Kwa hivyo, tutaona kwamba Biblia inafundisha kwamba yuko Mungu mmoja, mwenye nafsi mbili—Baba na Kristo—na wengine wengi zaidi kuongezewa baadaye. Mara ya kwanza Mungu atakapoongeza wana wengi katika Familia Yake ni pale ufalme wa Kristo unaposimamishwa. Lakini kuuingia ufalme wa Mungu halitakuwa jambo la moja kwa moja kwa mtu yeyote.
Yako Masharti Kuuingia Ufalme
Tunasoma katika sehemu kadhaa ambapo Kristo alisema ni wale tu wanaoshinda ndio watakaourithi ufalme na kutawala pamoja Naye. Kuna zaidi ya kuwepo katika ufalme wa Mungu kuliko kuutamani tu. Kuna MASHARTI ya kufuzu ambayo lazima yatimizwe.
Yesu alimwaambia kijana tajiri aliyeuliza kuhusu uzima wa milele, “…ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri” (Math. 19:17). Alifafanua kwamba mtu ni sharti azishike Amri Kumi ili aweze kuokolewa, na akanukuu tano kati yake.
Sasa dhambi ni nini? Kwa kuwa kuitenda huleta mauti (Rumi 6:23), si ni vyema ukajua ni nini? 1 Yohana 3:4 imerekodi, “Dhambi ni uvunjaji wa sheria.” Hii ni sheria ile ile ambayo kijana tajiri aliambiwa ni sharti aitii ili aweze kuurithi uzima wa milele.
Wengi hudai kuwa Wakristo—kuwa wafuasi wa Kristo. Wanadai “kumwamini Kristo” na hudai kuwa “watafutaji wa ukweli,” wakati hawataki ukweli halisi wa Biblia kabisa. Angalia majibizano haya marefu ambayo Yesu Kristo aliyafanya na Mafarisayo: “Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini [hawa walikuwa “waumini”], Ninyi mkikaa katika NENO LANGU, mmekuwa wanafunzi Wangu kweli kweli; tena mtaifahamu KWELI, nayo hiyo KWELI itawaweka huru…lakini mnatafuta kuniua kwa sababu NENO LANGU halimo ndani yenu…Lakini sasa mnatafuta kuniua Mimi, mtu ambaye nimewaambia ILIYO KWELI, niliyoisikia kwa Mungu…Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda Mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu...Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia NENO LANGU… Nami, kwa sababu nasema iliyo KWELI, hamnisadiki [bado inasema “walimwamini”]...Nami nikisema KWELI, mbona ninyi hamnisadiki?” (Yohana 8:31-32, 37, 40, 42-46). Yesu anaendelea katika maelezo kwa kuwashutumu kwa wazi wale ambao watadai kuwa Wakristo wakati kwa hakika ni “wa baba (yao) ibilisi.”
Wengi hudai kuwa “wanamjua Yesu” wakati kwa hakika hawajui chochote juu ya Kristo wa kweli wa Biblia. Kama alivyosema, kwa hakika “hawawezi kusikia” maneno ya Kristo—KWELI—ingawa wanaweza kufikiri kuwa wanasikia: “Yeye asemaye, NIMEMJUA, wala hazishiki amri Zake, ni mwongo, wala KWELI haimo ndani yake” (1 Yohana 2:4). Ulimwengu umejawa na mamia ya mamilioni ya “Wakristo” wa aina hii, wakifuata aina ya Yesu, lakini hawaijui kweli.
Wengi wasiouishi Ukristo, hujiingiza katika Kanisa la kweli. Lakini hatimaye wote huondoka. Yohana aliendelea, “Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu” (fu. 19). Nimeliona hili mara nyingi. Wengi wanaonekana kuamini juu ya Kristo, si kumwamini Yeye hakika—yaani kuamini kile alichokisema, na akasema KUTENDA!
Kumbuka maneno ya Kristo katika Marko 1:15: “TUBUNI, na kuiamini injili.” Toba ni kutoka dhambini (Matendo 3:19). Mkristo ni yule aliyegeuka kutoka—ametubu—dhambi zake, na amebatizwa (2:38) na kuongoka (3:19). Kwa maisha ya kushinda dhambi, Mkristo hufuzu kwa (ingawa hawezi kuchuma) wokovu na kuzaliwa katika roho kuingia ufalme wa Mungu.
Uwezekano Wako wa Kustaajabisha
Kumbuka Mungu alisema kwamba aliwaumba wanadamu kwa “sura” na “mfano” Wake. Fungu hili humaanisha kile linachokisema. Mungu alikuumba wewe ili uwe “kama” Yeye kwa kila namna. Kwa njia ya Roho Yake kuingia katika mawazo ya kila mtoto Wake mpya aliyeongoka, maisha mapya kabisa ya roho yametungwa. Katika wakati huo, “kiinitete” kidogo cha roho-kilichotungika hutokea, kikiwa tayari kukua na kuendelea katika mwonekano mzima wa roho, kwa mantiki hiyo tunaweza kusema, kwanza “kijusi,” kisha kuzaliwa.
Agano la Kale na Jipya kwa pamoja huweka wazi kabisa jambo hili! Wakati baadhi wana uelewa usio dhahiri kwamba Wakristo kwa namna fulani, wanakuwa “wana wa Mungu,” hakuna aliyewahi kufikiria jambo hili: “Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana NAYE; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1 Yohana 3:2). Tafakari maarifa haya ya kuduwaza, yasiyojulikana karibu na wote wanaojidhani kuwa Wakristo! Siku moja tutafanana kabisa na Kristo. Warumi 8:16 inasema kwamba sisi ni “watoto” wa Mungu na “warithi” pamoja na Kristo.
Mfalme Daudi pia alielewa jambo hili miaka elfu moja mapema alipoandika, “Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe KWA SURA YAKO” (Zab. 17:15). Bila kutegemea, fungu hili huondolea mbali wazo la “njozi nzuri” ya kufikirika iliyosambazwa na kanisa la ulimwengu—kwamba watu hawatauona uso wa Mungu katika maisha yajayo. Daudi alielewa kwamba tutamwona Mungu—na uso kwa uso. Vivyo hivyo Yohana. Wote walielewa kuwa, kwenye Ufufuo—“tutakapoamka”—tutakuwa kamili kama Mungu, katika umbo na tabia.
Kwa hivyo, Mungu anazaliana Mwenyewe katika wanadamu ambao wamepokea Roho Yake Takatifu. Anaumba watoto watakaofanana Naye kwa kila namna!
Lakini Petro aliandika kwamba ni lazima Wakristo “WAKUE katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo” (2 Petro 3:18). Wakristo wanapaswa—na lazima—wakue katika maisha haya ya sasa. Ili wapewe mamlaka ya kiungu na nguvu, kama warithi-pamoja na Kristo, lazima wafuzu, kwa kujenga tabia takatifu ya haki ya Mungu katika maisha yao.
Paulo alifafanua kwamba jukumu la mtumishi mwaminifu katika Kanisa ni kulilisha kundi. Yesu alisema, “Nitalijenga Kanisa Langu” (Math. 16:18). Ni Kanisa—Kanisa LILE—ambalo ni “Yerusalemu wa juu…mama yetu sisi” (Gal. 4:26; Ebr. 12:22-23). Kama alivyo mama yeyote, Kanisa hutunza na kulisha watoto wake—na amekuwa akifanya hivyo kwa miaka 2,000. (Jukumu la Kanisa kama mama yetu litafafanuliwa zaidi katika Sura ya Kumi.)
Andiko la Kustaajabisha
Kitabu cha Waebrania kinafunua Kusudi la Mungu la kustaajabisha kwa uwazi kama kioo. Muktadha huanza katika Sura ya 1. Tazama picha ya wokovu ikifunuka.
Kwanza, elewa kwamba Mungu aliumba malaika wawe “roho watumikao” wakitumwa kuwahudumu wale “watakaourithi wokovu” (fu. 14). Hili ndilo jukumu lao katika mpango wa Mungu. Malaika hawajapewa nafasi ya kuwa wanakaya [memba] katika Familia ya Mungu. Hii ndiyo sababu Shetani (kama malaika aliyeanguka) anachukia sana wazo kwamba wanadamu wa nyama, wadhaifu, wa hali ya chini wanaweza kupokea kile ambacho hakikutolewa kwake wala hawezi kukipata.
Paulo ananukuu sehemu mbili katika Zaburi: “Kwa maana Alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe Mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa Kwake Baba, Na Yeye atakuwa Kwangu Mwana?...” (fu. 5). Kamwe Mungu hajawahi kusema hili kwa malaika yeyote!
Kisha Paulo ananukuu zaburi nyingine, akifafanua kile ambacho kimekuwa kusudi la Mungu: “KITI Chako CHA ENZI, Mungu, ni cha milele na milele; Na fimbo ya UFALME Wako ni fimbo ya adili…” (fu. 8). Fimbo hutumika kama alama ya utawala au mamlaka—na katika ufalme Wake ni Mungu aliye na nguvu zote.
Mwisho, Paulo analiuliza swali lile lile kwa namna nyingine kuhusu malaika: “Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono Wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui Zako chini ya Miguu Yako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?” (fu. 13-14).
Hii inaweka jukwaa kwa ajili ya kile ambacho lazima tukifahamu! Hebu tutafakari vilivyo mustakabali wa kustaajabisha ambao Mungu ameandaa kwa ajili ya wale wote wanaomtumikia.
Mfululizo wa mafungu ya kushangaza unaendelea katika sura ya 2. Paulo alimnukuu Daudi (kutoka Zaburi 8:4-6) alipouliza swali hilo la muhimu-kuliko yote, “Mwanadamu ni nini hata Umkumbuke?” (fu. 6). Kwa kuwa Mungu ni wa milele, na huketi juu ya ulimwengu wote na ndiye mwenye uweza wote chini Yake, sio ajabu Daudi aliuliza, na Paulo akarudia, swali hili lilio kiini cha maisha.
Jibu la kushangaza huanza katika fungu linalofuata: “Umemfanya [mwanadamu] mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono Yako.”
Hatimaye Mungu atashiriki utawala wa uumbaji Wake wote na Wana Wake. Kwa mara nyingine, Kristo ni wa kwanza tu wa Wana wengi. Kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza hakuzuii kuzaliwa kwa wana wengine (na mabinti) kwa familia hiyo. Ninao wana wawili na mimi ni mzaliwa wa kwanza wa kiume nikiwa na kaka mdogo. Baba yangu alikuwa kijana wa pili, akiwa na kaka yake na kuendelea.
Paulo anaendelea kufafanua kwamba Mungu anapanga kuwapa Wana Wake nguvu nyingi ajabu na mamlaka: “Umeweka VITU VYOTE chini ya miguu yake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza KITU kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake” (fu. 8). Bado hili halijatokea—lakini litatokea hivi karibuni.
Mungu anaposema kwamba “vitu vyote” vitawekwa chini ya miguu ya mwanadamu, hicho ndicho anachomaanisha! Ulimwengu usiopimika, pamoja na mamilioni kwa kipawa cha nne cha nyota na trilioni moja ya galaksi, vitawekwa chini ya mamlaka ya wanadamu watakaokuwa wamezaliwa katika Familia ya Mungu. Kwa hakika, tafsiri ya Biblia ya Moffatt hulitafsiri neno la Kigiriki “vitu vyote” kama “ULIMWENGU.”
Kwa kweli haya ni maarifa ya kuduwaza! Tumia muda kuyashika. Furahia kile ambacho kinaweza kuwa mustakabali WAKO!
Kabla ya kuendelea, angalia fungu la kushangaza kuhusu kipengele kingine kinachohusiana cha wokovu ambacho hakikueleweka kabla. Tumeona kwamba Wakristo wanasubiri wokovu wa kustaajabisha ajabu. Lakini uumbaji kwa ujumla nao unasubiri kwa hamu kubwa kufunuliwa kwa wale wana wapya watakaoongezwa kwenye Familia ya Mungu. Soma mafungu yafuatayo kwa uangalifu kutoka Biblia ya Revised Standard Version:
“Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote [vitu vyote katika ulimwengu unaojulikana] pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari Yake, ila kwa sababu Yake Yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa WATOTO WA MUNGU. Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote [kila kitu] pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe [Wakristo] tulio na malimbuko ya Roho, sisi [WACHACHE wanaoitwa sasa] pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia [kufanywa] wana” (Rumi 8:19-23).
“Wana wote wa Mungu” wajao hatimaye watauweka huru uumbaji ambao sasa uko utumwani, na uliotabiriwa kuendelea kuwa mbaya zaidi. Dunia iliyooza na kujeruhiwa, jua, mwezi na nyota—ulimwengu!—utafanywa upya hivi karibuni na kurudishwa kwenye hali ya uzuri, usawa na utulivu chini ya uongozi wa Kristo na watakatifu waliofufuliwa.
“Kuleta Wana Wengi Kwenye Utukufu”
Sasa tunaweza kuendelea na maelezo ya muhimu sana katika Waebrania 2: “Ila twamwona Yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa Yeye, ambaye kwa ajili Yake na kwa njia Yake vitu vyote vimekuwapo, akileta WANA WENGI WAUFIKILIE UTUKUFU, kumkamilisha Kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso” (fu. 9-10).
Aya hii inafunua uwezekano wa kushangaza uliopangwa kwa ajili ya Wakristo wote. Wakati Kristo atakaporudi, Paulo anafunua kwamba watakuwepo “WANA WENGI” watakaoufikilia “utukufu” kwa njia ya “Kiongozi mkuu wa wokovu wetu.”
Fungu la 11 husema kwamba Kristo “haoni haya kuwaita [wale wana wengine wengi—sisi] ndugu.” Hawa ndio wale ambao kwao Kristo huitwa “mzaliwa wa kwanza.” Kwa kweli, mtu aliyetungwa ameitwa kuufikilia “utukufu” na kuwa mmoja wa “wana wengi.” Mateso na dhabihu ya Kristo ndivyo vinavyomfanya kuwa “Kiongozi mkuu wa wokovu wao”—na awezekanaye kabisa kuwa wako!
Ni uwezekano wa kustaajabisha namna gani kwa wale ambao Kristo anawaita…ndugu.” Sasa angalia fungu hili la mwisho: “Maana Yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii Haoni haya kuwaita ndugu” (fu. 11). Kristo na watakatifu wanashiriki wokovu ule ule.
Fungu hili linaonyesha kwamba Wakristo “wametakaswa” (tengwa). Kwa namna gani? Yohana anasema, “Uwatakase [Wakristo waliotungwa] kwa ile kweli; NENO LAKO NDIYO KWELI” (Yohana 17:17).
Tamaduni na hadithi zinazoshabikiwa na wanadamu, kuhusu maisha baada ya kifo au kitu kingine chochote, huanguka vinapochunguzwa. Wakristo, wakiwa wametoka kwenye ulimwengu uliodanganyika na kukanganyikiwa, wametengwa kutoka ulimwenguni kwa ile KWELI!
Kama Kristo “haoni haya kuwaita (sisi) ndugu,” hivyo basi sisi, wana wa Mungu waliotungwa, lazima tusione haya kuitetea ile kweli inayotutakasa—na kweli ya injili (Fil. 1:17). Ni lazima “tukue” kwa Kristo (Efe. 4:13) na tuyashike mafundisho ya kweli ya Mungu. Ni lazima TUFUZU ili siku moja tusimame kando ya Kristo juu ya “vitu vyote.”
Sasa rudi nyuma. Unakiona kilichoelezwa hapa? Lengo la kushangaza la Mkristo ni kuzaliwa katika ufalme wa Mungu—kufanyika nafsi roho AKITAWALA chini ya Kristo, kama mwana halisi wa Mungu. Kipi chaweza kuwa cha ajabu zaidi—cha UTUKUFU zaidi!—kwa ajili ya Mkristo kukitazamia?
Kristo Anarudi
Mathayo 24:27 inasema kwamba Kristo atakaporudi, Kuja Kwake kutakuwa kama umeme uking’aa kutoka mashariki hata magharibi. Hili litakuwa ni tukio litikisalo dunia yote, isiwezekane kulikosa.
Danieli aliongea juu ya Kristo kuja katika “mawingu ya mbinguni” (7:13). Kabla ya Kurudi Kwake, Mungu anampa rasmi MAMLAKA kutawala ulimwengu. Watakatifu hawawezi kupewa mamlaka na Kristo mpaka Yeye atakapopewa mamlaka kwanza. Hapo ndipo atakapoweza kuwapa nguvu wengine. Angalia: “Naye AKAPEWA [Kristo] mamlaka, na utukufu, na UFALME, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka Yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na UFALME Wake ni ufalme usioweza kuangamizwa” (fu. 14).
Lakini wajibu wa Mkristo katika maisha haya ni KUFUZU kuwa sehemu ya ufalme wa Mungu. Si ajabu Kristo alisema, “Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, naye atawachunga kwa fimbo ya chuma…kama Mimi nami nilivyopokea kwa Baba Yangu” (Ufu. 2:26-27) na mafungu machache baadaye, “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi…” (3:21). Kristo atakaporudi, watakatifu watawala pamoja Naye!
Msisimko wa maisha ya milele utakuwa hauna maelezo. Tutakuwa na uweza wa Mungu, kamwe hatutajisikia kuchoka, mateso, maumivu au uovu wa aina yoyote ile. Matazamio ya miradi mipya, mafanikio ya kustaajabisha na furaha isiyosemeka vitadumu milele.
Nani ambaye asingeyataka haya? Kwa nini mwanadamu hakuwahi kujua kwamba hii imekuwa HATIMA yake wakati wote—kwamba mateso yote na kukata tamaa kwa mwanadamu vingeweza kuondoshwa, kama mwanadamu angefahamu asili ya hulka ya mwanadamu, chanzo cha uovu wa kila namna—na kuishinda?
KWA NINI ulimwengu uko katika vurugu ya kutisha kama ulivyo? KWA NINI mwanadamu aliahidiwa uzima wa milele, bado akaumbwa kwa mavumbi ya ardhi—wa kufa—awezaye kufa? KWA NINI—na kwa jinsi gani—anatofautiana na wanyama? KWA NINI yeye anaweza kufikiri na kuwaza—kutatua matatizo na kupata jawabu—ili hali wanyama hawawezi? KWA NINI mawazo ya mwanadamu yana uwezo zaidi kuliko ubongo wa mnyama yeyote? Tofauti kati yao ni nini hasa?
Endelea kusoma ili kupata MAJIBU DHAHIRI ambayo wanasayansi, wanateolojia, wanafalsafa na waelimishaji wameyakosa!