Katika mwaka 1979, mwandishi mmoja wa gazeti aliwasiliana na mchungaji aliyekuwa akihudumia kundi kubwa la Kanisa huko Marekani ya Kaskazini-Mashariki akiomba kufanya mahojiano na mchungaji pia kuhudhuria kwenye ibada. Mahojiano hayo na kile ambacho angekiona kwenye huduma za siku ambayo angehudhuria vilitegemewa kutengeneza makala kwenye gazeti lake. Katika kipindi hicho Kanisa lilikuwa ndio kwanza limeanza kujulikana kitaifa na watu wengi hawakuwa na uelewa juu ya yale linayoyaamini.
Hata hivyo, makala hiyo haikuonekana kwenye toleo la Jumapili la gazeti hilo kama iliyoahidiwa. Akishangaa ni kwa nini, mchungaji alimpigia simu yule mwandishi, ambaye alikiri kwamba dhamira yake ya awali ilikuwa ni kulishtaki Kanisa kama kikundi cha kidini chenye msimamo mkali, lakini hakuwa tena na nguvu za kufanya hivyo. Alipoulizwa ni kwa nini, alifafanua kwamba baada ya kuona watu wengi walio marafiki na wenye furaha vilimmaliza nguvu, na hii ikamfanya kuacha na makala yake.
Kanisa hili pia lilifanya mikutano mikubwa na mingi kuliko yote ulimwenguni kila mwaka kwenye maeneo zaidi ya 120. Kila mahali Kanisa lilipokusanyika liliacha mvuto wa aina yake. Mfano mmoja: Kikosi cha Doria katika jimbo la Georgia kilichopangiwa kwenye eneo la mkutano katika kisiwa cha Jekyll, kilisema kuwa ilikuwa rahisi kuwaongoza washiriki wa Kanisa zaidi ya 10,000 kuliko mamia machache ya mkutano wa maofisa wa sheria uliokuwa karibu.
Ushirikiano wa washiriki wa mkutano na ukweli kwamba Kanisa liliweka viongozi wake wa misafara, maegesho na maafisa wa ulinzi ilimaanisha kwamba Kikosi cha Doria cha Jimbo la Georgia hakikuhitaji msaada zaidi. Mikutano mingine yote (pamoja na mkutano wa maafisa wa sheria) ilihitaji idadi kubwa zaidi ya walinzi wa Doria huku waliopewa jukumu la kuhakikisha taratibu zinafuatwa wakikumbana na ugumu katika kutekeleza majukumu yao.
Kila wakati na kila mahali waandishi wa habari walieleza kuwa ilikuwa ni furaha kuwa mwenyeji wa mikutano hii. Walifurahia kuona familia nyingi hivyo zenye maadili zikiwasili kwenye maeneo ya mikutano. “Si watu wa majigambo,” “wanyenyekevu,” “waliojaa furaha” na “watu wa-kweli wakionyesha amani iliyo ndani yao” ni baadhi ya kauli zilizotumika kulielezea Kanisa hili.
Kwa nini hali kama hii haipo katika ulimwengu wa leo? Kitu gani ambacho watu hawa walijua ambacho wengine wote hawakijui? Je, kuna mengine mengi zaidi kuliko yale yanayoweza kuonekana kwa macho?
Shauku ya Wote
Watu wote hutamani maisha tele ya furaha, amani. Lakini ni wa ngapi kwa hakika wanafurahia aina hii ya maisha yasiyokuwa ya kawaida?
Kuna mlipuko wa maarifa! Mwanadamu amefanikisha maendeleo ya kutisha katika utengenezaji wa vitu. Mavumbuzi katika sayansi na teknolojia hayajawahi kuwa makubwa hivi. Lakini je, wameweza kuleta maisha ya ukwasi, furi na furaha tele kwa watu wote? Je, elimu na mlipuko wa maarifa vimeyaleta? Je, dini imeweza kuleta maisha tele ya amani katika ulimwengu mzima? Je, serikali zimepata majibu kwa maswali makubwa ya mwanadamu? Je, viongozi wanaonyesha mfano unaoelekeza kwenye njia ambayo kwa hakika huleta furaha?
Kwa kila hali, jibu la wazi ni HAPANA!
Kupanuka kwa maarifa ya sayansi hakujaleta furaha ambayo viongozi walitabiri ingeambatana nayo. Wala nyenzo za kumpunguzia mwanadamu kazi, ambazo zilitegemewa kuwaletea wanadamu muda mwingi wa starehe ili “wajiburudishe” hazijaweza kufanikiwa.” Badala yake, magonjwa ya akili, mazoea ya kutumia madawa ya kulevya, kukata tamaa, kujiua, ulevi, kujihurumia, na aina nyingine za namna ya kutaka kujisahaulisha ugumu wa maisha, na kutoridhika na maisha kwa ujumla, vimejaa kila mahali.
Ufisadi na kumomonyoka kwa mwanadamu havijawahi kuwa katika hali mbaya zaidi kama ilivyo sasa. Dunia imejawa na matatizo—njaa, umaskini, machafuko ndani ya nchi, magonjwa, uchafuzi wa hali ya hewa, mkanganyiko wa kidini, vita, ughaidi, makosa ya jinai, madeni, ujinga na machafuko ya kisiasa. Na mambo huendelea kuwa mabaya zaidi.
Ndoa imeshambuliwa kuliko wakati wowote. Uzinzi unalipuka—kaya za asili na maisha ya familia yanafifia na yako katika hatari ya kutoweka. Idadi kubwa ya familia sasa zimevunjika, zimekanganyikiwa na hazina mwelekeo, huku mamilioni ya watoto wasiohesabika wakikua bila ya wazazi wote wawili. Mimba za utotoni na magonjwa yaambukizwayo kwa njia ya ngono yanaongezeka kwa kasi. Wazazi wanajiona hawana msaada katika kukuza watoto waadilifu katika ulimwengu wa sasa wa ufisadi.
Maelfu ya vita vimepiganwa katika jina la dini. Mamia ya mamilioni ya maisha yamefutika katika jina la amani! Na bado hakuna amani! Suluhu za kibinadamu daima hushindwa kuleta amani ya kudumu—mahali popote ulimwenguni.
Katika kila mzunguko, mwanadamu ameharibu juhudi zote za kutatua matatizo yake makubwa. Matokeo yake, wanadamu huteseka kutokana na kila aina ya uovu na ugonjwa. Maumivu, kukanganyikiwa, huzuni, kutoridhika, na hata kukata tamaa vinatawala.
Lakini iko njia ambayo huleta furaha ya kweli na amani. Baadhi wameipata njia ya maisha na wanaishi na kuifuata njia hii ambayo huleta shangwe, kuridhika, mafanikio—na kutosheka kwa daima.
Lakini, hii inahusisha wachache tu. Kwa nini? Jibu liko katika sheria msingi.
Sheria Kuu Isiyoonekana
Ziko sheria nyingi zisizoonekana zinazotawala maisha. Kwa mfano, kila mmoja anaifahamu sheria ya nguvu ya uvutano. Kama mtu kwa bahati mbaya atadondosha tofali juu ya mguu wake, matokeo yaweza kuwa mifupa iliyovunjika. Kama mruka angani ataruka kutoka kwenye ndege, na mwavuli ukashindwa kufunguka, matokeo ni kifo cha hakika. Hii ni rahisi kuelewa.
Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya sheria zisizoonekana ambazo nazo ni dhahiri. Kama mtu ni mgonjwa mara kwa mara, ni wazi kwamba sheria za afya (chakula sahihi, mazoezi ya kutosha, usingizi wa kutosha, n.k.) zinavunjwa. Athari ya afya mbovu ina sababu moja au zaidi. Kama ndoa itaishia kwenye kupeana talaka, inaweza pia kuwa ni kwa sababu moja au zaidi: kukosekana kwa mawasiliano, matatizo ya kifedha, kifo cha mtoto, matatizo ya unyumba, huzuni mahala pa kazi, n.k. Kama mtu atakamatwa kwa kuendesha akiwa amelewa, siyo vigumu kuona sababu za kukamatwa kwake.
Wengi hawatambui kanuni ya “sababu na athari” kama SHERIA kuu inayotawala karibu kila tendo maishani. Hawana habari kwamba hii ni kanuni ya kawaida inayotenda kazi ulimwenguni.
Kila aina ya athari inaweza kufuatiliwa hadi kwenye sababu moja au zaidi. Mimba zisizotarajiwa au haramu, makosa ya jinai, matumizi ya madawa ya kulevya, kufilisika, na athari zingine maelfu, zote zinaweza kuunganishwa kwenye sababu maalumu.
Lakini ni kwa nini mwanadamu haoni sheria hii ikifanya kazi anapoangalia ulimwengu katika ujumla wake au katika maisha ya mtu mmoja mmoja? Kwa nini dini pia zilipuuzia uhusiano huu kati ya sababu na athari?
Kuna sababu iliyo nyuma ya hali ya ulimwengu na ya wakazi wake.
Hata hivyo, tukilitambua hili, wako baadhi, waliotawanyika ulimwenguni, wanaoishi kwa furaha, maisha tele. Watu hawa wamesimama, waking’aa na furaha ya kweli, wakiwa na lengo katika maisha yao. Lakini hii si kwa sababu ya kisimati au habati—kuna sababu! Watu wengi hupuuzia sababu sahihi—na, matokeo yake, huvuna wingi wa athari mbaya.
Njia ya Maisha iliyojengeka Katika Mungu
Kuna sababu, itakayomfanya mtu kufikia mojawapo kati ya hatima mbili, ambazo huhusisha njia ya maisha ya mtu. Wale wachache wanaopitia maisha ya furaha hufuata njia ya Mungu. Ni washiriki wa Kanisa la Mungu, linalojulikana leo kama Kanisa la Mungu Rejeshwa, lililoelezewa mwanzoni mwa kijitabu hiki. Kila mshiriki amedhamiria KUUISHI Ukristo!
Inaweza kusemwa kuwa ziko njia mbili za maisha. Mojawapo inaweza kuelezewa kama njia ya “KUTOA”—njia ya upendo na kuwajali wengine—Njia ya Mungu! Nyingine ni kinyume chake au njia ya “KUPATA”—njia ya ubinafsi na kujijali mwenyewe—njia ya ulimwengu huu. Kwa miaka 6,000 mwanadamu ameishi njia hii moja—njia ya kupata.
Watu wengi wanapenda kufurahia starehe na kujikusanyia mali. Kama ilivyoonekana, “maisha ni kuona nani anaweza kufa akiwa nazo zaidi.” Hii inaweza kuwa kweli kwa ulimwengu huu, lakini si kweli kwa njia ya Ukristo.
Kristo alifundisha, “Ni heri KUTOA kuliko kupokea.” Kuishi njia hii ya maisha hupelekea kwenye wingi, amani, mafanikio, furaha ya kiwango cha juu na raha ambayo wote hutafuta. Kanisa la Mungu Rejeshwa hufuata njia hii hii ambayo Kristo na mitume wa awali waliifundisha.
Sheria ya kiroho ya Mungu—iliyofupishwa katika Amri Kumi—inaweza kutengwa katika mafungu mawili ya msingi: (1) Upendo kwa Mungu, kama ulivyofafanuliwa katika amri nne za kwanza. Kristo alizifupisha katika Mathayo 22:37: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote” na (2) upendo kwa wanadamu wengine, iliyofupishwa kwenye amri sita za mwisho: “Mpende jirani yako kama nafsi yako” (fu. 39).
Kutekeleza—kuishi!—Njia ya Mungu ndiyo SABABU ya furaha ya wale walio katika Kanisa hili. Kila mshiriki, akiwa amejawa na nguvu kwa Roho Mtakatifu, amedhamiria kuishi njia ya KUTOA—njia ya maisha iliyojengwa katika Mungu. Kanisa la Mungu Rejeshwa ni muunganiko wa mwili wa watu uliolenga kuleta tofauti katika maisha ya mtu mmoja mmoja. Unakusudia kuwasaidia wengine, kuwafundisha njia hii.
Furaha ambayo Wakristo wa kweli huipitia siyo ya juu juu, furaha feki. Hutiririka kutoka ndani ya maisha ya kila mshiriki. Kwa nini? Kwa sababu njia ya maisha iliyojengwa katika Mungu huleta hili!
Mungu—Muumbaji wa maisha yote duniani—alimpa mwanadamu kitabu cha maelekezo ya kina kilicho na habari nyeti, kikifafanua sisi ni nini, kwa nini tuko hapa na tunakwenda wapi. Wakati vitabu vya maelekezo na kiada vya taasisi za elimu ya juu huwafundisha wanafunzi namna ya kuwawezesha kuishi, aliyemtengeneza mwanadamu humfundisha namna ya kuishi, kupitia Neno Lake—Biblia Takatifu. Watu wa Mungu wamejitoa kufuata Neno Lake na kuishi kwa kila kanuni inayotoka humo. Wanaishi kanuni hizi na kupata matokeo yake—ndoa na familia zenye furaha, maisha ya kuzalisha na kazi, kuridhika na ukamilifu.
Lakini vipi kuhusu sehemu ya ulimwengu iliyobaki? Tujiulize tena, kwa nini kuna maovu mengi sana leo? Kwa nini makosa ya jinai yanaongezeka, misukosuko, maasi, vita na ghasia? Kwa nini upotovu unalipuka? Kwa nini zaidi ya nusu ya ndoa katika jamii ya sasa zinashindikana?
Ustaarabu umeshindwa—umepuuzia kikamilifu—habari nyeti!
Maarifa Yalipotea
Ubinadamu umepoteza maarifa ya njia ya Mungu ya maisha na namna ya kuiishi. Mwanadamu hajui kwa nini yuko hivyo, yeye ni nini na anakwenda wapi. Jamii imepoteza ufahamu ambao huleta furaha na raha. Haijui njia ya amani (Rum. 3:17; Isa. 59:8).
Kwa nini hali iko hivi?
Japokuwa hii inaonekana ni rahisi, sababu ya matatizo yote ya dunia ilianza katika Bustani ya Edeni. Mungu alikuwa ameshaumba vitu vyote na alikuwa ameshamfundisha Adamu lipi ni jema na baya ni lipi—lakini Adamu alisisitizia juu ya kuamua kati ya jema na baya yeye mwenyewe. Ubinadamu umefuata maamuzi ya Adamu—na njia—na umejawa na huzuni tangu hapo!
Ulimwengu umepoteza uoni kwa uamuzi uliofanywa na Adamu na Hawa. Hawakuchagua kula Mti wa Uzima, ambao Mungu aliwaambia wanaweza kula wakati wowote, badala yake wakachagua kula mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Kurudia kilichokwisha semwa, tangu hapo ubinadamu umefuata nyayo zao—njia ya KUPATA.
Hii inafafanua ulimwengu wa leo uliojawa na matatizo, maovu na magonjwa! Ujuzi na ufahamu wa Njia ya Mungu ukawa umepotea.
Tangu Uumbaji, mpaka Kuja kwa Kristo Mara ya Kwanza, ni wachache tu waliofuata maelekezo ya Mungu kuhusu mema na mabaya. Mtoto wa Adamu Habili alichagua njia sahihi ya maisha. Vizazi kadhaa baadaye, Henoko alitembea na Mungu. Mjukuu wake mkuu Nuhu alikuwa mtu pekee katika wakati wake aliyemfuata Mungu. Mtoto wake Shemu alifuata katika nyayo zake. Mara baada ya gharika, kulikuwa na Ibrahimu, baba wa waaminifu. Waliomfuatia walikuwa ni Isaka, Yakobo na Yusufu.
Wakati wa Musa, Mungu aliinua taifa lake, Israeli. Alifanya agano na Waisraeli, lakini mara baada ya muda mfupi, waliasi. Wakati Mungu akijaribu kuwafanya Waisraeli wafuate Njia Yake, walimkataa. Wakati huo huo, walimwengu wengine waliendelea katika njia ile ya kwanza ambayo Adamu na Hawa waliichagua.
Huu ulikuwa ulimwengu kabla ya Kristo—ambao ndani yake ni watu wachache pekee walitembea na Mungu. Karibia watu wote walikuwa wameasi, na maarifa juu ya Njia ya Mungu yakawa yamepotea kwa walio wengi. Huu ulikuwa ulimwengu uliohitaji Mwokozi ili aupatanishe kwa Muumbaji wake. Ni katika kipindi hiki ambapo manabii wengi walileta habari njema ya Masihi ambaye angekuja mara ile akileta ujumbe kwa ulimwengu.
Mjumbe na Tangazo Lake
Wakati huo Yesu hakuja kuuokoa ulimwengu na kutawala kama Mfalme, lakini kama Mjumbe mwenye tangazo. Ujumbe wake ulikuwa ni injili—HABARI NJEMA—ya kuja kwa ufalme wa Mungu.
Ili kutangaza ujio wa ufalme wa Mungu, Kristo alipaswa kumshinda Shetani, mungu wa ulimwengu huu. Ushindi huu ndio ungemfanya kufuzu kuchukua mahali pa Shetani na kuwa Mfalme katika ufalme wa Mungu unaokuja hivi karibuni.
Pia alikuja kuupatanisha ubinadamu kwa Baba. Tokea muda ule Adamu na Hawa walipomkataa Mungu, ubinadamu ukawa umekatwa kabisa kutoka kwa Mungu—na kutoka kwa maarifa ya njia ya kutoa, ambayo huleta mambo mazuri maishani. Akiwa mkamilifu, Kristo alitoa maisha yake kwa ajili ya binadamu. Kwa kafara yake—kifo Chake—Alilipa adhabu kwa ajili ya dhambi za wote.
Ufalme ambao Kristo aliutangaza ni serikali ya ulimwengu ya Mungu Mwenyezi, inayokuja hivi karibuni, itakayotawala mataifa yote na kuleta amani na mafanikio ya milele. Ujumbe huu wa injili ulihusisha ukweli kwamba, panapo toba na imani, watu wanaweza kuwa wana wa Mungu waliotungika. Kisha, baada ya maisha ya kushinda, kukua na kutoa, watoto hawa waliotungika wataweza siku moja kuzaliwa mara ya pili, wakiingia ufalme wa Mungu.
Kuzaliwa Kwa Kanisa na Kazi ya Mungu
Yesu alifahamu na aliwaambia wanafunzi wake kwamba yeye Mwenyewe hawezi kufanya jambo lolote. Roho wa Mungu alimwezesha kutimiza yote aliyoyatenda. Kabla hajapaa kwenda mbinguni, Kristo aliwaambia wanafunzi wake angewatumia Roho wa Mungu.
Tukio hili, kuanza kwa Kanisa la Mungu, lilitokea mwaka 31 B.K. Yesu alielezea umuhimu wa tukio hilo: “Lakini mtapokea nguvu, akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu: nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Wakati huo Mungu alitoa Roho wake Mtakatifu kwa wanafunzi 120.
Vile vile Kazi ya Mungu ilianza wakati huo huo. Kutangaza injili kwa ulimwengu—HABARI NJEMA ya ufalme wa Mungu ujao—injili ya kweli!—ndiyo imekuwa Kazi ya Mungu wakati wote! Wakiwa wamejawa na Roho Mtakatifu, watu wa Mungu sasa walikuwa wamewezeshwa kutimiza wito Wake.
Yesu alitamka, “Nitalijenga Kanisa Langu.” Hii huenda mbali zaidi ya kuanzisha, kuliongeza na kulitunza. Liko kusudi kubwa lipitalo ufahamu wa mwanadamu kwa ajili ya Kanisa ambalo Kristo alilijenga!
Kazi ya Mungu—Misheni
Kanisa la Kristo lina wito maalumu (misheni). Kila mshiriki ameitwa kuwa sehemu ya Kazi ya Mungu yenye kusisimua.
Misheni hii—Kazi hii ya UPENDO—ina maagizo ya aina mbili. Agizo la Kwanza ni “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15). Agizo la Pili ni kulilisha kundi la wanakondoo wa Mungu—kumpatia chakula cha kiroho kila mshiriki wa Kanisa la Mungu (Yohana 21:15-17). Kadri washiriki wa Mungu wanavyolishwa, wanakua kiroho, kukua huku kunawaruhusu kutumika na kujitoa wenyewe zaidi kwa Agizo Kuu la Kwanza.
Kutimiza Agizo la Kwanza leo ni jambo gumu kuliko ilivyokuwa katika enzi zile walizoishi mitume wa awali. Hata hivyo, kufundisha katika zama za habari inasisimua zaidi. Kiwango kikubwa sana cha maarifa husafiri kwa kasi isiyoweza kuelezewa. Ndani ya habari hizi yako maarifa ya njia ya Mungu ya maisha. Kanisa la Mungu Rejeshwa linaeneza injili katika kiwango na ufanisi ambao kanisa halijawahi kuona hapo kabla. Idadi kubwa ya watu sasa wanaweza kujifunza mambo mengi kadri watakavyo, wakati wowote wanapotaka. Mamilioni wengi ulimwenguni kote wanajifunza kanuni zilizothibitika, moja kwa moja kutoka katika Biblia zao, zikiwasaidia kuishi maisha ya furaha zaidi na kuwa raia wema.
Kanisa la Mungu Rejeshwa ni chemchemi ya maarifa ya kweli katika ulimwengu mkavu unaohangaika na maovu yanayoongezeka zaidi na zaidi.
Jina la Kanisa la Mungu
Usiku ule wa kusalitiwa kwake, Kristo aliliombea Kanisa: “Baba Mtakatifu, kwa JINA LAKO ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao duniani, mimi naliwalinda KWA JINA LAKO.”
Katika sehemu kumi-na-mbili tofauti, Agano Jipya limeandika kwamba Kanisa la kweli limelindwa katika jina la Baba—Mungu. Kila moja hutumia usemi “Makanisa ya Mungu.” Hili ndilo jina la Kanisa la Mungu!
Kanisa hili linaelewa umuhimu wa jina lake. Kama vile jina lilivyokuwa muhimu enzi za mitume wa awali, vile vile ni muhimu leo. Kulikuwa na nyakati katika Agano Jipya ambapo jina “Kanisa la Mungu” liliunganishwa na usemi wenye maelezo. Kwa mfano, “kwa Kanisa la Mungu lililoko Korintho.”
Katika zama hizi, kwa sababu za ushirika, Kanisa linaweza kutumia usemi kielelezo kujitambulisha lenyewe kutoka kwa “Makanisa ya Mungu” mengine. Tulichagua jina Kanisa la Mungu Rejeshwa.
Kristo ndiye kichwa cha Kanisa lake. Ila, Kanisa lake haliko mahali fulani lakini ni mwili wa kiroho unaoundwa na watoto wengi waliotungika. Likiwa limejawa na Roho Mtakatifu, likiwa na jina la Mungu, na likiongozwa na Kristo, Kanisa na Kazi yake vililipuka baada ya kuanzishwa kwake katika mwaka wa 31 B.K.
Mitume walikuwa wamejitoa kwa Kazi ya Mungu, kama lilivyo Kanisa la Mungu Rejeshwa leo hii.
Kusita Kwa Kazi
Chini ya uongozi wa mitume, ukuaji wa awali wa kanisa ulikuwa wa kuvutia mno (ubatizo wa watu 3,000 siku ya kwanza). Lakini mara baada ya kizazi cha kwanza cha Kanisa, Kazi ilianza kusita. Ilikosa msukumo kwa sababu ya mateso ya Warumi na shinikizo kutoka kanisa tofauti lililokuwa linaibuka.
Kipindi chote cha Zama za Kati, kazi ilizorota na onyo lake kwa ulimwengu likafifia. Lakini haikufa. Kristo aliahidi kuwa Kanisa lake halitakufa kamwe! Mwanzoni mwa karne ya ishirini, wakati uhai wa Kanisa na Kazi vilipokuwa vinadhoofu, zama mpya ikawa imewasili. Wakati ulikuwa umewadia kwa ujumbe wa Mungu wa wakati wa mwisho kwenda ulimwenguni kote.
Zama Mpya—Maisha Mapya
Katika majira ya kipupwe mwaka 1926, Mungu alimwita, na mara hiyo akaanza kumtumia, mwanaume aliyeitwa Herbert W. Armstrong (1892-1986). Aliliongoza Kanisa la Mungu kwa miaka 52, kuanzia 1934, aliposimamisha Redio Kanisa la Mungu (baadaye aliliita Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima).
Kuwasili kwa karne ya ishirini na moja, ilikuwa ni kufika kwa wakati ambapo ujumbe wa Kristo uende ulimwenguni kote. Chini ya uongozi wa bwana Armstrong, zama mpya ikaibuka, iliyofanana na Kanisa la karne ya kwanza. Ilikuwa ni zama yenye uhai, iliyoshuhudia ukuaji mkubwa wa Kanisa kwa ulimwengu mzima, na msisitizo ukiwa ni kuishi na kushiriki njia ya KUTOA. Likiwezeshwa na Roho Mtaktifu wa Mungu, Kristo aliye hai alikuwa Kichwa chake. Kadri muda ulivyopita, Mungu alirejesha kwa Kanisa mafundisho yote yaliyokuwa yamepotea karne zilizopita. Pamoja na mafundisho hayo lilikuwepo fundisho maalumu la ujumbe wa injili ya kweli.
Ujumbe huu, uliohafifishwa kwa karne nyingi, sasa ukawa umehuishwa!
Mizizi ya Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima
Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima hufuatilia historia yake mpaka kwa Kanisa lenye kutunza Sabato lililoanzishwa na Steven Mumford mwaka 1664 nchini Marekani. Mumford alikuwa ni mshirika wa familia ya Stennett wa Uingereza aliyekuwa ameongoza vuguvugu la watunza Sabato nchini humo miaka ya 1600. Watunza Sabato wa Kiingereza walifuatilia mizizi yao hadi kwa Walollards wa Uholanzi. Walollards nao walitoka kwa Wawaldensia watunza Sabato, ambao waliishi kabla ya karne ya 11 katika maeneo ya Alpini ya Ufaransa na Italia.
Nukuu ifuatayo huthibitisha kumbusho na maandishi ya imani ya Wawaldensia: “Njia ambayo Allix ameifuata katika Historia yake ya Makanisa ya Piedmont, ni kuonyesha kwamba katika historia ya dini kwa kila karne, kuanzia ya nne, anayoifikiria kuwa ni kipindi kizuri kwa yule anayetafuta kujua baada ya mafundisho safi ya mitume, kuna ushahidi wa wazi kwamba mafundisho…yalihifadhiwa na wanatheolojia wa kaskazini mwa Italia mpaka kipindi ambapo Wawaldensia walionekana kwa mara ya kwanza. Kwa ajili hiyo mawazo ya Wawaldensia hayakuwa mapya kwa Ulaya katika karne ya kumi-na-moja au ya kumi-na-mbili na hakuna kitu cha kutilia shaka katika mapokeo, kwamba Kanisa la Subalpine lilihifadhi kwa uaminifu kwa namna ya kuendelea tangu kuhubiriwa Injili kwa mara ya kwanza katika mabonde” (Gilly, Tafiti za Wawaldensia, uk. 118-119)
Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima
Kazi ya Mungu ililipuka, Milango ilifunguka kwa Kanisa kadri lilivyojitahidi kwa bidii kueneza ujumbe wa injili ya Kristo.
Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima lilikua kwa wastani wa 30% kila mwaka kwa miaka 35 ya kwanza—1934-1968. Hii iliwezesha Kazi ya Mungu kuvuma ulimwenguni.
Katika mwaka 1934, matangazo ya Ulimwengu wa Kesho kwa njia ya redio yalisikika kwa mara ya kwanza. Yakianza kwa kiwango kidogo, kwenye kituo kimoja cha redio chenye wati 100, kipindi kiliendelea kukua na kufikia vituo 400 vya redio na luninga, kikikadiriwa kuwa na wasikilizaji takribani milioni 250!
Ukweli Dhahiri—jarida lenye ufahamu lililotolewa bure—lilichapishwa kwa mara ya kwanza Februari 1934. Gazeti hili lilishughulika na masuala ya ulimwengu, maadili ya familia, afya na elimu sahihi. Tena, hili pia lilianza katika kiwango kidogo, kwa nakala 250 zilizochapishwa. Lakini, sauti ya Kristo ilikuwa nyuma ya ujumbe wa jarida la Ukweli Dhahiri ambalo lilikua na kufikia watu milioni 8.27 waliojiandikisha kutumiwa katika ulimwengu mzima, likikadiriwa kuwa na wasomaji takribani milioni 25.
Katika mwaka 1947, Kanisa lilianzisha chuo. Chuo kilihitajika ili kuipatia Kazi ya Mungu iliyokuwa inapanuka watumishi walioelimika. Baada ya muda, Kanisa likawa limeanzisha vyuo vitatu, vilivyolenga kuleta tofauti katika maisha ya wanafunzi wake—vikiwafundisha namna ya kuishi, siyo tu namna ya kupata kipato cha kuendeshea maisha.
Vijitabu kuhusu miadi, ndoa, uvutaji, madawa, kutawala mambo binafsi ya fedha, sheria za mafanikio, uongofu halisi na vingine vilitolewa bure kwa watu wengi sana. Wasomaji walifundishwa namna ya kuishi!
Kadri Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima lilivyoendelea kupanuka, maisha ya wengi yaliguswa. Mamilioni walisoma na kusikia ukweli wa njia ya Mungu ya maisha. Walianza kuelewa kwamba kuna njia nyingine—maisha ya kutoa—njia ya maisha iliyojengeka katika Mungu. Wengi waliokuwa nje ya kanisa walishiriki faida ya elimu hii ya ajabu.
Lakini, kama vile kazi ilivyosita kizazi kimoja baada ya kuanza kwa Kanisa la karne ya kwanza, ndivyo pia ilisita baada ya kifo cha bwana Armstrong.
Historia ya Kanisa ya Hivi Karibuni
Katika harakati ya kihistoria, viongozi waliomfuatia bwana Armstrong hatimaye walibadilisha mafundisho yake yote. Kadri muda ulivyokuwa unapita, ikaonekana wazi kuwa Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima lilikuwa halikui, bali linapungua. Ukuu na mvuto wa ujumbe wa Mungu ulio wazi na wenye nguvu ukafifia.
Jambo hili lilisababisha makundi kadhaa kujitenga kutoka kwa kanisa hilo. Lakini makundi yote yaliyojitenga yalikuwa yamekubali baadhi ya mabadiliko katika mafundisho yaliyofundishwa na uongozi mpya wa Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima.
Wale walioona hitaji la kushikilia imara mafundisho yote ya awali, kufuata kwa ukamilifu Sheria ya Mungu ya Upendo (1 Yohana 5:3; Rumi 13:10), waliona kwamba makundi yote yalikuwa yamekubaliana na baadhi ya mabadiliko. Wakiwa na shauku ya kuhifadhi kanuni yote kama ilivyo, ambayo ndiyo iletayo ile amani ya ajabu, furaha na maisha tele, Kanisa la Mungu Rejeshwa lilianzishwa. Wale walioshikilia ukweli wote waliendelea kuongozwa na Kristo, akiwaruhusu kuiendeleza kwa mafanikio Kazi ya Mungu iliyo tukufu na yenye uvuvio.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa, David C. Pack, aliyepakwa mafuta katika Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima, na akitumika katika utumishi tangu 1970, akaja kuona kwamba hakuna kiongozi au kundi lililoshikilia mafundisho yote ya awali ambayo bwana Armstrong aliyafundisha. Binafsi akiwa amefundishwa na bwana Armstrong, bwana Pack alielewa hitaji la kuendeleza misheni kama alivyofundishwa na kuufikia ulimwengu wote na ujumbe huo huo wa injili. Chini ya uongozi wake, Kanisa la Mungu Rejeshwa lilizaliwa.
Historia Fupi ya Kanisa la Mungu Rejeshwa
Kujiunda huku upya kwa Kanisa la Mungu kulianza mwezi Mei 1999, lililosimama si kama chipukizi la Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima, lakina kama mwendelezo wa Kanisa kama lilivyoanzishwa awali—likiendeleza huduma ya mitume wa awali na mafundisho.
Kanisa la Mungu Rejeshwa lilianza katika mazingira ya hitaji la msingi la kufundisha habari njema—INJILI—ya ufalme wa Mungu Mwenyezi unaokuja hivi karibuni. Yale tunayoyaamini ni imani ile ile “iliyotolewa awali kwa watakatifu.” Kristo habadiliki kamwe, wala mafundisho ya Kanisa Lake!
Kimsingi miaka kadhaa ya mwazo wa uwepo wa Kanisa la Mungu Rejeshwa ilikuwa ni maandalizi kwa ajili ya kuendeleza Kazi ambayo bwana Armstrong alikuwa ameianzisha. Wakati Kanisa halikupuuzia kulilisha kundi, zana zote ambazo Kanisa lilizitumia hapo awali—vitabu na vijitabu vitolewavyo bure, masomo ya Biblia, makala, majibu mafupi kwa Maswali & Majibu, majarida na matangazo ya hewani, na mpango wa usambazaji—vilianzishwa.
Kanisa hili limejizatiti kufuata njia ya Mungu ya maisha na kudhamiria kutimiza Agizo la Kwanza—kuufikia ulimwengu na injili ya Kristo—kufundisha njia sahihi, iliyo tofauti sana na njia ya ulimwengu ya kupata.
Kazi ya Mungu Katika Karne ya 21
Kama lilivyokuwa Kanisa la karne ya kwanza, ndivyo lilivyo kanisa hili kwamba halina ama mamilioni ya washiriki wala nguvu zozote za kisiasa au kidini au mvuto.
Bado, tunatambua hitaji la kuusambaza ujumbe wa Mungu—kuufikia ulimwengu unaotaabika, unaoteseka. Wakati urithi ulianza na mitume wa awali, Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima lilifuata nyayo zake, na Kanisa la Mungu Rejeshwa linaendelea leo. Ujumbe ni ule ule na lengo ni hilo moja—njia tu hutofautiana.
Tovuti ya Kanisa la Mungu Rejeshwa (rcg.org): Kanisa la Mungu Rejeshwa linaendesha tovuti ya kibiblia iliyo kubwa kuliko zote Duniani, ikibeba machapisho mengi na yanayoongezeka ili kuwaongoza watu wanaotafuta kuishi njia ya Mungu ya maisha. Bado, tofauti na makanisa mengine, hakuna cha kununua wala kulipia. Vyote ni bure bila gharama.
Nguvu ya mtandao wa intaneti ni ya kustaajabisha, ikituruhusu sasa kuzifikia nchi na maeneo 220, na kwa hakika hakuna nchi ambayo haijafikiwa, isipokuwa kufikiwa kwa nguvu kubwa na matokeo makubwa. Idadi ya watu tunaoweza—na tutakao—wafikia hakika ni kubwa ajabu. Jambo hili limekuwa la kutia moyo kwa wale wanaosaidia Kazi hii.
Programu ya Ulimwengu Ujao™ (rcg.org/worldtocome): Ikirushwa kupitia mtandao wa intaneti, programu hii hujibu maswali kama: Ulimwengu unakwenda wapi? Kwa nini umejawa na matatizo, machafuko, maovu na maradhi, yakisababisha huzuni, kukanganyikiwa na taabu za kila namna? Kinachokuja mbele ni nini? Katika zama za hofu, mkanganyiko na kukosa matumaini, Ulimwengu Ujao ni sauti ya ukweli, ikitoa majibu, na kutangaza tumaini kwa ubinadamu!
Katika mwaka 1934, wakati programu ya Ulimwengu wa Kesho iliporushwa hewani kwa mara ya kwanza, iliweza kuanza kwenye kituo kimoja tu. Leo, programu ya Ulimwengu Ujao inapatikana muda huo huo ulimwenguni kote!
Jarida la Ukweli Halisi™ (rcg.org/realtruth): Pia tunachapisha jarida ambalo linaendeleza ujumbe wa jarida la Ukweli Dhahiri. Jarida la Ukweli Halisi limesheheni makala zinazofafanua sababu ya vita, kuna tatizo gani na hali ya hewa, je, sayansi itaweza kutokomeza uchafuzi wa mazingira, maana ya matukio katika Ulaya, kwa nini matetemeko ya ardhi yanaongezeka, kushindwa kwa sayansi kuleta maisha makamilifu
ambayo kila mmoja anayatamani, namna gani ubaguzi wa rangi hatimaye utatoweka, uchumi wa dunia unaelekea wapi, nini kinachokuja mbele ya mataifa ya dunia, thamani ya maadili mema—na fasili ya tabia ya kweli, sababu haswa ya kuporomoka kwa maadili katika nchi za Magharibi, kuna tatizo gani na elimu ya leo, kwa nini wengi wanatafuta mikato na starehe, na fasili ya mafanikio ya kweli.
Tulifafanua juu ya ulimwengu kukosa viongozi maarufu na kile kitakachochukua nafasi zao, na jinsi ambavyo amani itakuja katika wakati wetu, namna ya kujenga familia imara—kulea watoto wenye furaha na wazalishaji—namna ya kumaliza mashaka yako ya masuala ya kifedha, kwa nini magonjwa mapya yanaibuka na ya zamani yanarudi—yakiwa makali zaidi kuliko hapo kabla—na kama Umoja wa Mataifa kweli ni jibu sahihi kwa ubinadamu.
Tunafafanua kwa nini kuna maelfu ya aina za Ukristo—zinazotofautiana—na zisizokubaliana, kwa nini dini haijatatua matatizo makubwa ya ulimwengu, namna ya kuielewa imani halisi, namna ya kumtambua Kristo halisi wa Biblia, njia ya “kutoa” dhidi ya njia ya “kupata,” sheria ya sababu na athari, kiini cha asili ya ubinadamu, kanuni za maisha yenye afya, na mafundisho mengine mengi. Jarida linaleta ufahamu ulio dhahiri wa matatizo yasiyo na majibu yanayomlemea mwanadamu, na linaonyesha ilipo amani ya kudumu ya ulimwengu ujao, ng’ambo ya upeo wa macho.
Likiwa na zana hizi na zaidi, Kanisa la Mungu Rejeshwa linasaidia watu ambao sasa wanazama katika bahari ya matatizo. Wengi wanapata MAJIBU, na wanajifunza kuyafanya maisha yao yawe ya furaha na yanayozaa matunda.
Namna Gani Inategemezwa?
Kanisa la Mungu Rejeshwa kamwe halishawishi umma ulichangie fedha.
Tumejitolea kwa dhati kwenye wito huu wa UPENDO—wa kuwajali watu wote ulimwenguni kote. Kazi zetu zote zinategemezwa na watu wanaotoa. Tukifuata agizo la Kristo katika Mathayo 10:8, “Mmepokea bure, toeni bure,” tunatoa kila kitu bure.
Kanisa la Mungu Rejeshwa hupokea zaka zinazolipwa kwa hiari na washiriki wake. Wanatambua mibaraka tele iliyoahidiwa na Mungu kwa wale wote watakaotii sheria yake ya utoaji wa zaka. Faida ya ziada wanayoipata watu wanaotekeleza sheria hii isiyokuwa ya kawaida ni kwamba inawasaidia kupangilia vizuri mambo yao binafsi ya kifedha. Hatima yake, Kanisa na watu wake wanafanikiwa kutokana na kutekeleza sheria hii iliyothibitishwa kutoka kwa Neno la Mungu. (Wako wengine wanaochangia mara kwa mara kama watendakazi wenza na wafadhili, nao wakitaka kushirikiana na wengine kile ambacho wamepokea.)
Stahiki Yetu Ni Wapi Katika Ulimwengu?
Kristo hakuja duniani akiwasihi watu wawe waongofu, badala yake alikuja na tangazo lililoelezewa mapema kwenye kijitabu hiki. Alifundisha njia ya maisha ambayo ulimwengu ulikuwa umeikataa na kuisahau. Hakuja kuuokoa ulimwengu wa wakati wake. Alikuja kutangaza wakati ujao ambapo ulimwengu wote utaokolewa. Tunafuata mfano wake.
Mfano wa Kristo, na ule wa mitume, huonyesha kwamba Wakristo hawashawishi watu wabadili dini. Kanisa la Mungu Rejeshwa pia linafuata kanuni hii. Hatujaribu kuuongoa au kuutengeneza ulimwengu huu, badala yake tunaendeleza ujumbe wa tangazo la Kristo. Kanisa la Mungu Rejeshwa linafafanua nini hakiendi sawa ulimwenguni pasipo “kuhubiria” watu au kuwahukumu. Tunatoa tumaini, tukionyesha ni namna gani hatimaye shida za mwanadamu zitakavyotatuliwa. Tunaleta hamasa na uhai kwenye mada zilizo katika mawazo ya watu leo—tukieleza sababu za mlipuko wa matatizo duniani. Tunafundisha “sababu na athari,” na siyo lundo la mapendekezo yanayofunika matatizo.
Wengi wanashagazwa kwamba matatizo na changamoto walizonazo maishani—zingine zikionekana hazitatuliki—zinaweza kutatulika kwa kufuata njia ya Mungu ya maisha. Kwa kumtanguliza Mungu katika kila jambo, maisha yanaweza kunyooka na yakawa yakuridhisha.
Kanisa la Mungu Rejeshwa halitoi mapendekezo ya kisiasa. Tena, halijihusishi kabisa na vuguvugu lolote la kisiasa au agenda. Badala yake linafundisha UPENDO—kuwajali wengine—watu wote ulimwenguni.
Ingawa kipaumbele cha Mkristo wakati wote ni kwa serikali na maagizo ya Mungu, Biblia inafundisha hitaji la kujisalimisha inavyostahili kwa serikali za wanadamu. Tunazingatia kwa nguvu sana fundisho hili.
Ukuaji wa Kushangaza
Mitume wa awali walikuwa ni kikundi kidogo sana ambao hatimaye walileta athari chanya kwa ulimwengu wa wakati wao. Vivyo hivyo Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima lilianza kama kikundi kidogo na, ndani ya nusu karne, lilikuwa na athari chanya kubwa kwa mataifa ya ulimwengu. Akiitwa Balozi wa Amani ya Ulimwengu, Herbert W. Armstrong binafsi alitembelea moja-ya-tatu ya wakuu wa nchi—wafalme, malkia, marais na mawaziri wakuu—wa wakati wake.
Wakati pia likianza kama kikundi kidogo, na bado siyo kubwa kwa viwango vya wanadamu, Kanisa la Mungu Rejeshwa nalo linashuhudia ukuaji imara na athari chanya kwa ulimwengu. Na pamoja na mtindo wa ukuaji ambao Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima lilishuhudia, Kanisa la Mungu Rejeshwa litaendelea kukua na kusonga mbele zaidi, likiwasidia watu wengi kwa kuwapa maarifa nyeti ya kiroho, na likisababisha mabadiliko chanya katika maisha ya wengi zaidi.
Kristo aliwaamuru wanafunzi wake kwenda ulimwenguni kote. Tunafanya vivyo hivyo! Tukileta ujumbe wa njia ya Mungu ya maisha hata kwa nchi za mbali kama Zimbabwe, Iceland, China, Chile, New Zealand, Misri, India na Ulaya yote. Hii haijakoma—na sasa kwa uthabiti tunafikia mataifa yote duniani!
Makumi ya maelfu hutembelea tovuti zetu kila siku. Watu wanafundishwa kanuni za kweli za njia ya maisha yenye kuzalisha. Sasa wana silaha za maarifa yanayoweza kuwasaidia kukua na kuwa mifano bora—na raia wema—katika jamii zao.
Kanisa la Mungu Rejeshwa linatoa tumaini. Zana kama matangazo ya kurusha hewani, majarida matatu, vitabu, vijitabu, vipeperushi, makala na masomo ya Biblia (vijana na wakubwa) vinaathiri maisha ya watu ulimwenguni. Maelefu wanajifunza Mungu yupo na kwamba liko tumaini halisi kwa ulimwengu! Idadi ya watu wanaojifunza njia inayopelekea afya na maisha tele—furaha halisi—imekuwa ikikua kwa uthabiti kila juma. Tunalenga kusaidia na kutoa kwa faida ya maisha ya mtu mmoja mmoja.
Athari na Mabadiliko
Mitume wa awali walijitahidi kuleta tofauti. Kanisa la Mungu la Ulimwengu Mzima lilifanya tofauti katika maisha ya mamilioni. Kanisa la Mungu Rejeshwa nalo lina moto
huo huo—tumaini lile lile—kudhihirisha mfano chanya na kwa huo kuwa na athari chanya kwa ulimwengu. Nalo pia linafanya tofauti halisi.
Makutano makubwa walifikiwa na mafundisho ya kweli ya Kanisa chini ya Herbert W. Armstrong. Ujumbe huu huu unaendelea leo—na matunda ya Kazi ya Mungu yanathibitika!
Kupitia intaneti na Programu yetu ya Utawanyaji wa Habari ulimwenguni kote, maelfu wanafikiwa. Familia nyingi zinafundishwa kanuni za kuwa na ndoa zenye furaha, na wanajifunza namna ya kulea watoto katika ulimwengu uliopoteza maarifa hayo ya msingi. Pia watu wanajifunza juu ya sheria zinazoleta mafanikio halisi na ya kudumu. Maisha yanabadilika—watu wanaguswa katika njia chanya.
Nguvu ya Roho wa Mungu inaondoa kukata tamaa na kuleta nguvu na tumaini. Inaleta hamasa kufanikisha, na kuondoa mkanganyiko na kukosa mwelekeo. Inachukua ndoto zilizogandamizwa na hisia zilizosinyaa, na kuzipanua katika upeo mkubwa ajabu—na kuvuvia mategemeo ya mafanikio. Inachukua mfadhaiko na kuubadilisha uwe uzalishaji na MAFANIKIO yanayoridhisha.
Karibu hakuna mtu afahamuye Ukristo ni nini hasa. Wengi hawana habari kwamba unaweza kuwaletea furaha ya kiwango cha juu, zaidi ya inavyoweza kufikiriwa. Hawana wazo kwamba Ukristo huwakilisha ukamilifu, utajiri, starehe na kujawa na wingi, kimwili na kiroho.
Kristo alisema, “Nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yohana 10:10).
Msisimko, furaha, hamasa na kuridhika kunakotokana na ufahamu huu huhafifisha kila jaribu, ugumu, kikwazo, kizuizi na tatizo ambalo mtu anaweza kukumbana nalo. Kwa kweli kuelewa hili kunapelekea kujua kwa nini Yesu alisema kwamba NJIA YAKE inawakilisha maisha ya ajabu zaidi—tele zaidi—zaidi ya wengi wanavyoweza kufikiria!
Wengi wanaishi maisha yaliyojaa hamasa, juhudi, shauku na msukumo—na yakiongozwa na tumaini na imani—kana kwamba mafanikio ya mwisho hutegemea utendaji wao wa kila siku.
Hiki ni kiasi kidogo tu cha matunda yanayokua katika maisha ya watu wanaodhamiria kuishi kwa kila neno la Mungu (Math. 4:4; Luka 4:4).
Washiriki wa Kanisa wamejitoa kuangaza nuru yao katika ulimwengu wa “ki-leo” unaohitaji sana nuru! Katika ulimwengu unaotamani sana amani, ambao wakaazi wake wanaota ndoto ya maisha yenye mafanikio, tunatoa tumaini kwa kila anayesikiliza—ujasiri wa kina ulio ndani, uliotokana na uelewa kwamba maisha maangavu, yenye furaha yanawezekana, na kwamba ULIMWENGU WA KUSTAAJABISHA unakuja hivi karibuni.
Hili hapa ndilo Kanisa la Mungu Rejeshwa!