Watu wengi huendelea mbele kama walivyofundishwa, wakidhani ya kwamba kile wanachoamini na kukitenda ni sahihi. Wanachukulia tu kwamba imani zao ni sahihi. Wengi hawatumii muda kuthibitisha kwa nini wanatenda mambo wanayotenda.
Kwa nini unaamini kile unachoamini? Ulitoa wapi yale unayoyaamini? Je, asili ya mambo ya kidini unayoyaamini ni Biblia—au ni mamlaka nyingine? Kama unasema ni Biblia, je, una uhakika?
Vipi kuhusu Isita (Pasaka isiyokuwa ya Wayahudi)? Kwa kuwa mamia ya mamilioni wanaitunza, ikidhaniwa ni maadhimisho ya Kufufuka kwa Yesu Kristo, basi bila shaka lazima Biblia iwe na mengi ya kusema juu yake. Hakika kuna mafungu mengi yanayotaja sungura, mayai na utafutaji wa mayai, vikapu vya peremende, maandazi ya moto yenye alama ya msalaba, Kwaresima, Ijumaa Kuu na ibada za maawio ya jua—bila kutaja Isita yenyewe.
Isita inahitaji uchunguzi wa karibu na kijitabu hiki kinaichambua kwa makini.
Mamlaka ya Biblia Kwa Ajili ya Isita?
Biblia ndiyo asili ya mambo yote ya Kikristo. Je hutaja Isita? Ndiyo.
Angalia Matendo 12:1 [Biblia toleo la King James]. Mfalme Herode alianza kulitesa Kanisa, akiishia kumuua kikatili mtume Yakobo kwa upanga. Jambo hili liliwafurahisha sana Wayahudi kiasi kwamba mtume Petro naye akawekwa gerezani na Herode. Mpango ulikuwa ni kumtoa kwa Wayahudi baadaye. Fungu la 3 husema, “Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa.” Kanisa la Agano Jipya lilikuwa likitunza siku hizi za sikukuu zilizoelezewa kwenye Mambo ya Walawi 23. Sasa soma fungu la 4: “Alipokwisha [Herode] kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne [kumi-na-sita], wamlinde, akitaka baada ya Isita kumtoa na kumweka mbele ya watu.”
Je haya ni mamlaka ya Biblia kwa ajili ya Isita?
Aya hii haiongelei juu ya Isita. Tunajuaje? Neno lililotafsiriwa Isita [Biblia toleo la King James] ni neno la Kigiriki pascha (lililotokana na neno la Kiebrania pesach; hakuna neno la asili kwenye Kigiriki kwa ajili ya neno Pasaka (ya Wayahudi), na lina maana moja tu. Wakati wote humaanisha Pasaka—kamwe neno hili haliwezi kuwa na maana ya Isita! Kwa sababu hii, tunapata neno la Kiebrania lililotumika katika Agano Jipya kwa lugha ya Kigiriki. Kwa mara nyingine, neno hili la Kiebrania linaweza kumaanisha Pasaka tu. Na Tafsiri zingine za Biblia, kama Revised Standard Version, hutafsiri neno hili kwa usahihi Pasaka.
Badala ya kuidhinisha Isita, fungu hili huthibitisha wazi kwamba Kanisa lilikuwa bado linatunza kile kinachodhaniwa kuwa ni Pasaka ya Wayahudi miaka kumi baada ya kifo cha Kristo!
Hebu sasa tugeukie maandiko mengine yanayotoa mamlaka kwa Isita. Hii inaleta tatizo. HAKUNA maandiko yoyote! Kwa hakika hakuna mafungu, popote katika Biblia yanayotoa mamlaka au kupitisha utunzaji wa sherehe za Isita! Biblia haisemi chochote kuhusu Kwaresima, mayai na utafutaji wa mayai, vikapu vya peremende, n.k., japokuwa hutaja maandazi ya moto yenye alama ya msalaba na ibada za maawio ya jua kama machukizo, ambayo Mungu anayalaani. Tutayachunguza mambo haya na kujifunza kwa nini.
Tafsiri isiyo sahihi (kwenye Biblia inayoaminiwa sana ya King James Version) ya Matendo 12:4 siyo ujanja uliojificha sana katika kujaribu kuingiza sikukuu ya kipagani katika maandiko kwa lengo la kuihalalisha. Tutaichunguza Pasaka kwa ukaribu baadaye.
Pasaka (ya Wayahudi) Kwa Ufupi
Kisa cha Pasaka ya Agano la Kale kinachojulikana sana kimejikita katika ukombozi wa Mungu kwa Waisraeli kutoka Misri kwa njia ya mapigo kumi ya kimiujiza. Hii ni pamoja na jinsi malaika wa mauti “alivyopita juu” ya nyumba zote ambazo Waisraeli walikuwa wakiishi. Waliagizwa kupaka damu katika miimo ya milango ili kuhakikisha kwamba ni wazaliwa wa kwanza wa Misri pekee ambao wangekufa. Katika Pasaka hii ya kwanza, ni damu pekee ya mwanakondoo aliyechinjwa iliyolinda kila nyumba ya Mwisraeli. Wakati Misri ikipitia pigo la mauti, wazaliwa wa kwanza wa Kiisraeli walikombolewa kwa damu. Kwa kutii amri ya Mungu na imani katika ahadi Yake ya kuwalinda, waliokolewa kutoka mautini.
Maelezo ya Pasaka yanapatikana katika kitabu cha Kutoka 12:12-14. Fungu la 14 husema kuwa sherehe ya Pasaka iliamuriwa na Mungu kuwa sikukuu ya ukumbusho kila mwaka itakayotunzwa na Israeli “milele.” (Amri hii imerudiwa katika Mambo ya Walawi 23:5.) Kutoka 12:15 hutambulisha sikukuu ya siku saba inayoitwa Siku za Mikate Isiyochachwa (pia imerudiwa katika Mambo ya Walawi 23:6-8), ambayo ilifuata mara tu baada ya sikukuu ya Pasaka kila mwaka. Hii ndiyo sababu Matendo 12:3 husema, “Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa,” kabla ya kutaja Pasaka katika fungu lililofuata. Siku hizi zilitunzwa sambamba kila moja na nyingine.
Vipi Kuhusu Agano Jipya?
Kama Pasaka iliwekwa idumu milele, basi maagizo yake kuhusu kuitunza ni lazima yawe wazi katika Agano Jipya. Agizo hili linapatikana katika 1 Wakorintho 5:7-8: “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu [ya mikate isiyochachwa, ambayo wakati wote ilifuata baada ya Pasaka kama ilivyofafanuliwa hapo juu]…”
Kristo, kama Mwanakondoo wa Mungu (Yohana 1:29; Matendo 8:32; 1 Petro 1:19; Ufu.5:6), alichukua mahali pa mwanakondoo wa Agano la Kale aliyeliwa jioni ya siku ya Pasaka kila mwaka. Alama za Agano Jipya za mkate na divai ziliwekwa ili Wakristo waweze kula mwili na kunywa damu ya Kristo, aliye Mwanakondoo wa kweli wa Mungu. Dhabihu ya Kristo ilichukua mahali pa hitaji la kuua mwanakondoo wa majira ya machipuko. Luka 22:19 huonyesha kwamba Yesu aliingiza mkate na divai vitumiwe kila mwaka katika kumbukumbu ya dhabihu Yake kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu—za kiroho na kimwili pamoja.
(Soma kijitabu chetu cha bure Meza ya Bwana Ifanywe Mara Ngapi? Kinathibitisha Kristo hakubadilisha Pasaka na sikukuu nyingine! Pia, kinaweka wazi kwamba kitu pekee alichobadilisha ni mwanakondoo wa majira ya machipuko na dhabihu yake mwenyewe—na kuingizwa kwa mkate na divai kama kielelezo chake!)
Wakristo wa mwanzo walitunza Pasaka, siyo Isita. Angalia nukuu hii kutoka Ensaiklopidia ya Britannika, Toleo la 11, Kitabu cha 8, uk. 828: “Hakuna dalili ya kutunzwa kwa Isita katika Agano Jipya, au katika maandiko ya Akinababa wa Utume…Wakristo wa awali waliendelea kutunza sikukuu za Kiyahudi [siku kuu za Mungu kwenye Mambo ya Walawi 23], ijapokuwa katika upya wa roho, kama maadhimisho ya matukio ambayo siku kuu hizo ziliyaashiria. Kwa hiyo Pasaka, pamoja na maana mpya iliyoongezwa kwayo, ya Kristo kama mwanakondoo wake wa kweli…iliendelea kutunzwa.”
Mitume wa awali na Kanisa la kwanza la Agano Jipya hawakutunza Isita. Angalia: “Katika karne ya pili B.K., Siku ya Isita, miongoni mwa Wakristo katika Asia ndogo [bila shaka haya yalikuwa makanisa ya watu wa Mataifa ambayo Paulo aliyaanzisha katika maeneo kama Filipi, Kolosi, Galatia, nk.—na aliwaonya Wagalatia (4:9-10) kuhusu kutunza siku kama Isita] ilikuwa siku ya 14 ya mwezi wa Nisani [au Abib] ambao ni mwezi wa saba wa kalenda [ya kiserikali] ya Kiyahudi” (Shajara ya Mwaka ya Ulimwengu, toleo la 1968, uk. 187). Tarehe iliyoelezewa hapa siyo Siku ya Isita, bali ni Pasaka—ambayo ilitunzwa siku ya 14 ya mwezi wa kwanza (Nisani) ya kalenda takatifu. Mitume na Kanisa la kwanza hawakutunza Isita!
Pamoja na ushahidi mwingi kwamba Siku Takatifu za Mungu zilizoorodheshwa katika Mambo ya Walawi 23, zinatakiwa kutunzwa na Wakristo leo (Matendo 2:1; 12:3; 18:21; 20:6, 16; 1 Cor. 5:7-8; 16:8), lakini miongoni mwa wote wanaodai kumwamini Mungu wa Biblia karibu kabisa hakuna hata mmoja anayezitunza! Karibu kabisa hakuna hata mmoja anayedai kumwabudu Yesu Kristo anatunza Pasaka kama Alivyoamuru! Kwa nini?
Kwa kuwa agizo la kutunza Isita halimo katika Biblia, na amri ya Mungu ya kudumu kuitunza Pasaka ndio iliyomo, basi Isita ilichipukia wapi? Baada ya kupitia kwa ufupi asili ya Pasaka, tuko tayari kujifunza asili ya Isita.
Wakati Isita Ilipoingia Amerika.
Isita imejulikana kuwa ni sikukuu ya kipagani kwa kipindi kirefu! Waanzilishi wa Marekani walijua hili! Kitabu cha watoto kuhusu sikukuu hii, Gwaride la Isita: Karibu Kipindi Kitamu cha Majira ya Machipuko!, kilichoandikwa na Steve Englehart, uk. 4, husema, “Wakati Wapyuritani walipokuja Amerika ya Kaskazini, walitunza sherehe za Isita—na sherehe za Krismasi—kwa mashaka. Walijua kuwa wapagani walikuwa wakisherehekea kurudi kwa majira ya machipuko siku nyingi kabla Wakristo hawajaanza kusherehekea Isita…kwa miaka mia mbili ya kwanza ya maisha ya kiulaya katika Amerika ya Kaskazini, ni nchi chache tu, hasa katika Amerika ya Kusini zilizingatia sana Isita.” Ilikuwa ni baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ndipo Waamerika walianza kusherehekea sikukuu hii: “Isita ilikuwa utamaduni wa Waamerika Kwa mara ya kwanza kwenye miaka ya 1870” (uk. 5). Kumbuka! Makoloni 13 ya awali ya Amerika yalianza kama taifa la “Kikristo”, na kauli mbiu “Hakuna mfalme bali Mfalme Yesu!” Taifa halikuitunza Isita kwa karne nzima tangu kuanzishwa kwake. Nini kilitokea kikabadilisha hali hii?
Isita Ilitoka Wapi?
Je, usemi huu unaeleweka?—Majira ya machipuko yako hewani! Maua na sungura vinapamba nyumba. Baba anawasaidia watoto kuchora picha nzuri kwenye mayai yaliyochovya kwenye rangi mbali mbali. Mayai haya, ambayo baadaye yatafichwa na kutafutwa, yanawekwa kwenye vikapu vipya vizuri. Harufu nzuri ya maandazi ya moto yenye alama ya msalaba ambayo mama anaoka kwenye joko yanaijaza nyumba. Siku arobaini za kujinyima kula vyakula maalumu zitaisha siku inayofuata. Familia nzima inaandaa nguo zao nzuri za Jumapili watakazovaa kesho kwenye ibada ya maawio ya jua kusherehekea kufufuka kwa mwokozi na kufanywa upya kwa maisha. Kila mmoja anatazamia paja la nguruwe lililo teketeke pamoja na mapochopocho mengine. Itakuwa ni siku ya kusisimua. Kwani, ni siku moja muhimu sana ya sikukuu ya kidini ya mwaka.
Hii ni Isita, ama siyo? Hapana! Haya ni maelezo ya familia ya Kibabeli ya kale—miaka 2,000 kabla ya Kristo—wakiadhimisha kufufuka kwa mungu wao, Tamuzi, aliyerudishwa kutoka ulimwengu wa chini na mama/mke wake, Ishita (kutoka kwake jina la sikukuu lilipatikana). Kwa kuwa Ishita hakika ilitamkwa “Isita” katika ndimi nyingi za kisemitiki, kwa mantiki hiyo inaweza kusemwa kwamba tukio lililoelezewa hapa, ndio Isita. Bila shaka, tukio hili laweza kuwa ni familia ya Kifirijia ikimwadhimisha Attisi na Sibele, au pengine familia ya Kifoenike ikimwabudu Adonisi na Asitate. Tukio hili pia laweza kuwa familia ya Kiisraeli iliyoasi ikimwadhimisha Baali na Ashtorethi wa Kanaani. Au maelezo haya yanaweza kuwakilisha sherehe zingine chafu za kipagani za kufa na kufufuka—ikiwa ni pamoja na sherehe za Isita ya kileo maana imekuja kwetu kupitia matambiko ya uzazi ya Kianglo-Sakzoni ya mungu mke Ostire au Ostara. Hizi zote ni sikukuu zinazofanana, zikitenganishwa tu na wakati na tamaduni.
Ikiwa Isita haipatikani kwenye Biblia, basi ilitoka wapi? Wengi wa wanahitoria wa kibiblia na kiulimwengu wanakubaliana kwamba jina ‘Isita” na tamaduni zinazolizunguka zina mizizi iliyozama katika dini za kipagani.
Sasa angalia nukuu zifuatazo zinazodhihirisha zaidi kuhusu asili ya kweli na jinsi sherehe za kisasa za Isita zilikopata jina lake:
“Tangu Bede Mtukufu (De ratione temporum 1:5) asili ya neno kwa ajili ya sikukuu ya Kufufuka kwa Kristo limechukuliwa na walio wengi kuwa limetoka kwa mungu mke wa majira ya machipuko wa Anglo-Sakzoni Eastre…ambalo ni wingi wa neno eostarun katika Kijerumani Kikuu cha Kale likimaanisha mapambazuko; ndiko lilikotoka neno la Kijerumani Ostern, na neno la Kiingereza Easter” (Ensaiklopidia Mpya ya Kikatoliki, 1967, Kit. 5, uk. 6).
“Ukweli kwamba sikukuu za majira ya kumea zilikuwa za kawaida miongoni mwa wapagani hakuna shaka kwamba zilihusika sana na aina za sikukuu katika ukanda wa Mashariki zilizokuja kukubaliwa na makanisa ya Kikristo. Neno la Kiingereza Easter lina asili ya kipagani” (Albert Henry Newman, D.D., LL.D., Mwongozo wa Historia ya Kanisa, uk. 299).
“Katika sikukuu hii kubwa ya Kikristo, hujitokeza masalio kadhaa ya sherehe za kipagani za kale. Kwanza, jina lenyewe si la Kikristo bali la kipagani. Ostara alikuwa Mungu Mke wa Majira ya Machipuko wa Waanglo-Sakzoni” (Ethel L. Urlin, Sikukuu, Siku Takatifu, na Siku za Watakatifu, uk. 73).
“Isita—jina Isita limetokana na Ostera au Eostre, mungu mke wa majira ya machipuko wa Waanglo-Sakzoni, ambapo sikukuu ya majira ya machipuko ilifanywa kwa ajili yake kila mwaka, ni kutokana na sikukuu hii ya kipagani baadhi ya tamaduni zetu za Isita zimepatikana” (Hazeltine, uk. 53).
“Huko Babeli…mungu mke wa majira ya machipuko aliitwa Ishita. Yeye alifananishwa na sayari ya Venasi, ambayo, kwa sababu…[hu]ibuka kabla ya Jua…au huzama baada yake…huonekana kupenda mwanga [hii ina maana kwamba Venasi inampenda mungu-jua]…Huko Fonesia, akawa Asitate; katika Ugiriki, Eostre [likihusiana na neno la Kigiriki Eos: “mapambazuko”], na katika Ujerumani, Ostara [hili linatoka katika neno la Kijerumani Ost: “mashariki,” ambao ni upande wa mapambazuko]” (Englehart, uk. 4).
Kama tulivyoona, majina mengi yanaingiliana kwa kile kinachojulikana sana Isita. Ni wazi wapagani walitumia majina tofauti kwa ajili ya huyo huyo mungu au mungu mke. Nimrodi, mtu maarufu katika Biblia aliyejenga jiji la Babeli (Mwa. 10:8), ni mfano. Aliabudiwa kama Satuni, Vulkani, Kronosi, Baali, Tamuzi, Moleki na mengine, lakini wakati wote alikuwa mungu huyo huyo—moto au mungu wa jua kwa ujumla aliyeabudiwa karibu katika kila jamii ya watu wa kale. (Soma kijitabu chetu cha bure Ukweli wa Asili ya Krismasi kujifunza zaidi kuhusu sikukuu hii na sehemu ya Nimrodi ndani yake.)
Mungu mke Isita hakuwa tofauti. Alikuwa mungu mke mmoja na majina mengi—mungu mke wa uzazi, aliyeabudiwa kipindi cha majira ya machipuko wakati maisha yote yalikuwa yanafanywa upya.
Mwanahistoria anayejulikana sana, Will Durant, katika kazi yake maarufu na yenye kuheshimiwa, Simulizi ya Ustaarabu, ku. 235, 244-245, ameandika, “Ishita [Asitate kwa Wagiriki, Ashtorethi kwa Wayahudi], hutuvutia si tu kwa sababu ni sawa na Isisi wa Kimisri na mfano wa Afrodaiti wa Ugiriki na Venasi wa Kirumi, bali kama mrithi halali wa moja ya tamaduni ngeni za Kibabeli…anajulikana kwetu hasa kutokana na ukurasa maarufu katika kitabu cha Herodotus: Kila mwanamke mzawa analazimika, mara moja katika maisha yake, kukaa katika hekalu la Venasi [Isita], na kufanya ngono na baadhi ya wageni.” Je, ni ajabu kwamba Biblia huzungumzia mfumo wa kidini uliotokana na hilo jiji la kale kama, “SIRI, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI” (Ufu. 17:5)?
Ni lazima sasa tuangalie kwa ukaribu asili ya desturi zingine zinazoambatana na sherehe za Isita za nyakati hizi.
Asili ya Kwaresima
Kulingana na Johannes Cassianus, aliyeandika katika karne ya tano, “Hata hivyo unapaswa kujua, kwamba kadri ambavyo kanisa la awali lilivyoendelea na ukamilifu wake, utunzaji huu wa Kwaresima haukuwepo” (Mkutano wa Kwanza Abbot Theonas, sura ya 30). Hakuna kumbukumbu wala katika Biblia au historia ambapo Kristo, mitume au Kanisa la awali walishiriki katika majira ya Kwaresima.
Kwa kuwa hakuna maagizo ya kushika Kwaresima katika Biblia, ilitoka wapi? Kipindi cha siku arobaini za saumu zilishikwa siku za kale kwa heshima ya miungu ya kipagani Osirisi, Adonisi na Tamuzi (John Landseer, Tafiti za Kisebia, ku. 111, 112). Kitabu cha Alexander Hislops, Babeli Mbili, uk. 104-105, husema hili kuhusu asili ya Kwaresima: “Siku arobaini za saumu ya Kwaresima ziliazimwa moja kwa moja kutoka kwa waabudu wa mungu mke wa Kibabeli. Kwaresima hiyo ya siku arobaini, katika majira ya machipuko ya mwaka, bado inashikwa na Wayezidisi au waabudu-Shetani wa kipagani wa Koordisitani, ambao wameirithi kutoka kwa mabwana zao, Wababeli. Kwaresima hiyo ya siku arobaini ilishikwa wakati wa majira ya machipuko na Wapagani wa Kimeksiko…Kwaresima hiyo ya siku arobaini ilishikwa nchini Misri…”
Kwaresima ilitoka kwa upagani, sio kutoka kwa Biblia! (Ili kujifunza zaidi kuhusu kipindi cha Kwaresima, soma makala yetu “Maana ya Kweli ya Kwaresima.”)
Mayai, Uwindaji Yai na Isita
Wakati wote mayai yamehusishwa na sherehe za Isita. Karibu kila utamaduni katika ulimwengu wa leo wana kawaida ya kupaka mayai rangi kwa umaridadi na kwa njia tofauti tofauti. Niliwahi kuchunguza maonesho yanayotembezwa ya aina ngingi za mayai yaliyopambwa kiustadi ambayo yaliwakilisha mitindo na mila za kila nchi ya Ulaya ya leo.
Angalia aya ifuatayo: “Asili ya yai la Isita imejengwa juu ya mila za uzazi za jamii za Kiindo-Ulaya…Kwao yai lilikuwa ni alama ya majira ya machipuko…Katika nyakati za Kikristo yai lilikuwa limejaliwa tafsiri ya kidini, likawa ni ishara ya kaburi la mwamba ambalo kutoka kwake Kristo aliibuka na kuingia maisha mapya ya Kufufuka Kwake” (Francis X. Weiser, Kitabu cha Sikukuu na Desturi za Kikristo, uk. 233). Huu ni mfano wa moja kwa moja wa jinsi ambavyo alama na desturi za kipagani zinavyofanywa kuwa za “Kikristo,” yaani, majina yanayotamkika Kikristo yanabandikwa juu ya tamaduni za kipagani. Hii hufanyika ili kuwadanganya—vile vile kuwafanya watu wajisikie vizuri kuhusu kwa nini wanafuata desturi ambazo haziko katika Biblia.
Angalia: “Kuhusu ushikaji wa Isita wa Kikristo…desturi zinazoonekana zimejikusanya, nyingi ya hizo zikiwa zimerithishwa kutoka sherehe za kale…alama za sherehe za kipagani za majira ya machipuko za Kiulaya na Kimashariki ya Kati…kwa mfano, mayai…yamekuwa maarufu sana kama ishara ya maisha mapya na ufufuo” (Ensaiklopidia ya Britannika, toleo la 1991, Kit. 4, uk. 333).
Hatimaye, nukuu ifuatayo inatoka kwa Imani ya Kimisri na Mawazo Mapya, James Bonwick, uk. 211-212: “Mayai yalining’inizwa katika mahekalu ya Kimisri. Bunsen anatilia msisitizo kwa yai la kawaida, alama ya maisha yanayochipukia, likitokea mdomoni mwa mungu mkuu wa Misri. Yai la kisiri la Babeli, likiangua Venasi Ishita, lilianguka kwenye mto Frati kutoka mbinguni. Mayai yaliyopakwa rangi yalikuwa ni matoleo matakatifu ya Isita katika Misri, kama ambavyo bado yalivyo katika China na Ulaya. Isita au majira ya machipuko, yalikuwa ni majira ya kuzaliwa, viumbe vya nchi na vya mbingu.”
Kipi chaweza kuwa wazi zaidi katika kuonyesha asili ya ukweli wa “yai la Isita”? Yai la “Isita” ni yai tu linalohusishwa na Isita. Kamwe Mungu hakuamuru mayai ya Pasaka au mayai ya Siku za Mikate Isiyochachwa, lakini kumekuwepo na mayai ya Isita kwa miaka maelfu!
Iliendelea katika hali ya kawaida tu kwamba hilo yai, likiwakilisha majira ya machipuko na uzazi, lingeunganishwa kwenye sikukuu ya kipagani ya majira ya machipuko iliyokuwepo. Kuunganisha ishara hii na Kufufuka kwa Kristo wakati wa majira ya machipuko kulihitaji ubunifu zaidi na fikira za kibinadamu. Hata hivyo, hata ubunifu wa hali ya juu wa fikira za kibanadamu kamwe haujafaulu kuunganisha alama ya Isita inayofuata na chochote cha Kikristo, kwa maana hakuna hata neno moja juu yake popote katika Agano Jipya!
Sungura wa Isita
Hizi hapa ni nukuu mbili zaidi kutoka kwa Francis Weiser kuhusu asili ya “sungura wa Isita”: “Katika Ujerumani na Austria viota vidogo vyenye mayai, vitobosha na peremende huwekwa mahali pa siri, na watoto huamini kwamba sungura wa Isita, anayejulikana sana katika nchi hii, pia, alitaga yale mayai na kuleta peremende” (uk. 235) na “Sungura wa Isita alikuwa na asili yake katika mila za uzazi kabla ya Ukristo…Sungura wa Isita kamwe hajawahi kuwa na alama yoyote ya kidini iliyoidhinishwa kwa ajili ya matumizi katika sikukuu…Hata hivyo, sungura amepata jukumu la pekee katika sherehe za Isita kama mtengenezaji wa mayai ya Isita kwa ajili ya watoto katika nchi nyingi” (uk. 236).
Ufuatao ni uthibitisho zaidi wa asili ya mayai ya Isita na sungura. Unadhihirisha jinsi ambavyo hakuna yeyote aliyeweza kuunganisha sungura wa Isita na kitu chochote cha Ukristo, achilia mbali Biblia: “Sungura wa Isita siyo alama ya kweli ya Ukristo” (John Bradner, Alama za Majira na Siku za Kanisa, uk. 52), na “Ingawa imekubaliwa katika jamii kadhaa za Kikristo, sungura wa Isita hajawahi kupata tafsiri yoyote ya Kikristo” (Mirsea Eliade, Ensaiklopidia ya Dini, uk. 558).
Hakuna lolote kati ya haya litawazuia mamilioni ya wanaojiita Wakristo wasipambe mazingira na nyumba zao kwa sungura wa Isita kila majira ya machipuko.
Fikiria nukuu hii ya mwisho: “Sungura, alama ya uzazi katika Misri ya kale, alama ambayo ilishikwa baadaye katika Ulaya…Mahali pake pamechukuliwa na sungura wa Isita (Ensaiklopidia ya Britannika, tol. 1991. Kit. 4, uk. 333).
Hata katika nyakati hizi, sungura wamebaki kuwa alama ya uzazi. Ingawa kiwango chao cha kuzaliana haraka kinajulikana vyema, tatizo lingine linaibuka kuwahusu sungura—hawatagi mayai! Ingawa alama zote ni za uzazi, hakuna mantiki yoyote ya kuziunganisha. Katika ulimwengu uliojaa tamaduni za kipagani, ukweli na mantiki vinaweza kupotea. Kuziunganisha alama hizi na Ukristo hufanya jambo ambalo tayari ni tendo la ibada ya sanamu kuwa baya zaidi.
Hakuna kitu chochote cha Ukristo kuhusu yoyote ya alama hizi. Historia ya kweli kuhusu alama hizi za uzazi, mayai na sungura, haijulikani kabisa kwa watoto wote wasiotilia shaka ambao wameoongozwa na watu wazima kuzifikiria kwamba ni za pekee sana.
Dhana nzima kwamba hizi ni alama za Kikristo ni uongo ulioelekezwa kwa watoto wasio na hatia ambao wanaweza kuamini kuwa “mwezi umetengenezwa kwa jibini” kwa sababu mtu fulani tu atawaambia hivyo. Wakati hizi ni kweli zinazoshtua, kwa kweli ndivyo zilivyo.
Mwokozi Bandia?
Moja ya dhana kuu katika Agano Jipya ni kwamba Yesu Kristo alikuja kufa kwa ajili ya dhambi za wanadamu na kutoa ukombozi kwa ulimwengu uliokatwa kutoka kwa Mungu.
Mkuu wa kughushi (mwovu Shetani, aitwaye “mungu wa ulimwengu huu” katika 2 Kor. 4:4) hutafuta kughushi kila kipengele cha mpango wa Mungu. “Audanganyaye ulimwengu wote” (Ufu. 12:9). Akiwa mdanganyifu mkuu, asingeridhika kughushi vipengele vingine vya Ukristo na kuacha utambulisho na ibada ya Mwokozi wa kweli!
“Mwokozi” halisi katikati ya desturi ya “Jumapilii ya Isita” ni nani? Je, ni yule Yesu Kristo wa Biblia? Kama unasema “ndiyo,” una uhakika? Historia hujibu swali hili kwa wazi, namna hii:
Kwanza angalia kwamba: “…dhana ya Mungu-Mwokozi ilikuwa ni kitu cha kawaida katika ulimwengu wa kale wa kipagani…dhana ya wokovu ndiyo msingi wa fikira za miungu kama Osirisi, Attisi, na Adonisi…” (John M. Robertson, Ukristo na Mithiolojia (elimu ya visasili), uk. 395).
Kisha hii: “Mara nyingi imedaiwa kwamba imani hii katika Kufufuka kwa Yesu ni kwa sababu ya fikira za ufufuo wa kiungu zilizoko ulimwenguni sasa…simulizi za Attisi, Adonisi, na Osirisi…Katika simulizi za kipagani kufufuka tena ni upinduaji wenye furaha dhidi ya kushindwa, katika simulizi ya Kikristo ni kamilisho la kifo cha ushindi. Inaweza kusemwa kwamba Attisi na Osirisi waliokoa kwa kufufuka tena, Yesu kwa kufa…ushikaji wa Isita haukutokea mara moja kutokana na imani katika Ufufuo, bali ulianza baadaye kwa hatua za taratibu kutoka kwenye Pasaka ya Kiyahudi. Dhana inayomaanishwa katika salamu ya Isita Kristo amefufuka ni hatua ya pili ya maendeleo; fikira hii inatoka katika sikukuu hii sambamba na kutokea kwake katika majira ya machipuko; sikukuu haitokani na fikira. Fikira ya kufufuka kwake Kristo ilichomekwa katika kawaida za zamani za ushikaji wa Isita na si vinginevyo” (A. Nock, Ukristo wa Mwanzo wa Watu wa Mataifa na Msingi Wake wa Kihelenisti, ku. 105-107).
Na, hatimaye, dhana nzito ya bandia ambayo hurudiwa mara kwa mara imewekwa wazi zaidi na mwanahistoria maarufu, James George Frazer: “Sasa kifo na kufufuka kwa Attisi vilisherehekewa rasmi huko Roma tarehe 24 na 25 ya mwezi Machi, tarehe ya mwisho ikijulikana kama ikwinoksi [siku mlingano (ambapo jua huvuka mstari wa ikweta na usiku na mchana kuwa sawa)] ya majira ya machipuko, na…kulingana na desturi ya zamani iliyoenea sana kwamba Kristo aliteseka siku ya tarehe 25 ya mwezi Machi…desturi iliyoweka kifo cha Kristo siku ya tarehe 25 mwezi Machi…ni ya kushangaza zaidi kwa sababu maangalizo ya kinajimu huthibitisha kwamba isingeweza kuwa na msingi wa kihistoria…Tunapokumbuka kwamba sikukuu ya Mt. George katika mwezi Aprili imechukua mahali pa sikukuu ya kipagani ya kale ya Parilia; kwamba sikukuu ya Mt. Yohana Mbatizaji katika mwezi Juni imefuatia sikukuu ya kipagani ya maji iliyo katikati ya majira ya Mavuno; kwamba sikukuu ya Kupalizwa Bikra mwezi Agosti imeiondoa sikukuu ya Diana; kwamba sikukuu ya Watakatifu Wote [kufuatia mkesha wa sikukuu ya watakatifu wote (31 Oktoba)] katika mwezi Novemba ni mwendelezo wa sikukuu ya kale ya kipagani kwa ajili ya wafu; na Kuzaliwa kwa Kristo mwenyewe kuliwekwa kwenye mwanzo wa majira ya baridi mwezi wa Desemba kwa sababu siku hiyo ilidhaniwa ni Kuzaliwa kwa Jua; hatuwezi kufikiriwa kuwa na pupa au wasio makini katika kudhani kwamba sikukuu nyingine maalumu ya kanisa la Kikristo—uhalalishaji wa Isita—ulikuwa katika namna ile ile, na kutoka katika nia ile ile ya kurekebisha, kulikofanywa kwenye sherehe inayofanana na ya Attisi mungu wa Kifirijia siku ya 21 mwezi Machi wakati wa majira ya kumea…ni upatanifu wa kushangaza…kwamba sikukuu za Wakristo na watu wa Mataifa za kifo na ufufuo wa ki-mungu vyote vingeadhimishwa majira yale yale…ni vigumu kuufikiria upatanifu huu kama kitu ambacho hakikukusudiwa” (Tawi la Kidhahabu, Kit. 1, ku. 306-309).
Tunaweza kufanya muhtasari wa chanzo hicho hapo juu. Kanisa la Kikatholiki la Kirumi lilikuwa na kawaida ya kuingiza sikukuu za kipagani—kwa kuzipachika majina ya “Kikristo” na kuziita za “Kikristo.” Hii ilifanyika ili Ukristo ukubalike na ueleweke zaidi kwa wenye kuabudu miongoni mwa watu wa Mataifa, ambao Kanisa lilikuwa likijaribu kuwavutia. Ni kwa jinsi gani hali hiyo ya mambo ilianza?
Sasa inaweza kueleweka vizuri zaidi kwa nini mtume Paulo aliwaandikia Wakorintho wawe macho dhidi ya udanganyifu wa kijanja wa “Yesu mwingine ambaye hatukumhubiri.” Alisema, “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali…” (2 Kor. 11:3-4).
Leo watu wanaweza kufikiri kwamba wanamwabudu Mwokozi wa kweli wakati kwa hakika wanaabudu mwokozi bandia—Yesu mwingine! Kwa hakika Ukristo wote wa kawaida unamwabudu Baali, mpatanishi na mungu jua, aliyeitwa jina kufuatia “mke” wake Ishita (ambaye kwa hakika alikuwa mama yake Semiramisi)—tutakuja kuona baadaye kuwa ndiye yule Biblia humwita “Malkia wa Mbinguni.”
Watu wanaweza kuabudu katika njia zinazowakilisha vitu ambavyo ni tofauti kabisa na kile wanachokiamini kwa dhati au kukusudia. Tafakari mfano huu halisi.
Ibada za Maawio ya Jua
Ibada za maawio ya jua zimetajwa katika Biblia. Lakini kile ambacho Mungu anasema kuhusu desturi hii si kile unachotarajia. Angalia mafungu haya ya kushangaza. Nabii Ezekieli alikuwa akionyeshwa, katika njozi, unabii wa muhimu juu ya dhambi za watu wa Mungu katika wakati wetu.
Muktadha mzima wa mafungu haya unahitaji kuchunguzwa kwa uangalifu ili kuelewa laana kuu ambayo Mungu anaijenga kuelekea kwenye hitimisho Lake: “…Utaona tena machukizo makubwa mengine wanayoyatenda…na tazama, wanawake wameketi wakimlilia Tamuzi…Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya Bwana, na tazama, mlangoni pa hekalu la Bwana, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la Bwana, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki. Basi, akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! Ni jambo dogo…wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? Kwa maana…wamerejea nyuma ili kunikasirisha…Kwa sababu hiyo mimi nami nitatenda kwa ghadhabu; jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma, na wajapolia masikioni mwangu kwa sauti kuu, sitawasikiliza.” (Ezek. 8:13-18)
Kushika ibada za maawio ya jua ni jambo kubwa kwa Mungu! Anachukia sana kitendo hiki kiovu kiasi kwamba hatimaye atawaangamiza kabisa wale wote wanaodumu kuzifanya (Ezek. 9)!
Si “jambo dogo” kwa Mungu kwamba mamilioni wengi wanayafanya haya kila Isita! Inaweza kuonekana “maridadi,” “jambo la kidini”, na “linalogusa sana” kwa wale wanaolishiriki, lakini Mungu amewakataza watu wake wa kweli kubuni kawaida na fikira zao za kidini. Hapendezwi katika kile ambacho watu wanaweza kujisikia au kufikiri ni sahihi wao binafsi. Anapendezwa na wale ambao wanajali kile anachokifikiria! Kulingana na Mungu, ibada ya jua ya kale, iliyovishwa vazi zuri na kofia za Isita, ni namna ya ufungashaji wa kisasa wa desturi ya zamani sana, ambayo ni ibada ya sanamu ya kipagani.
Fikiria maneno ya Mungu mwenyewe katika Kumbukumbu la Torati 12:28-32: “Maneno haya nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza...Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali… nawe…kuketi katika nchi yao; ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata… wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, ‘Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo.’ Usimtende kama haya Bwana, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa Bwana, ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao...Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze.”
Mungu huwaambia Wakristo wasichanganye kilicho cha uungu na kilicho cha kipagani—au ukweli na uongo! Usikubali watu wakuambie kwamba kile asemacho Mungu hakifanyi tofauti. Kinafanya!
Maandazi ya Moto Yenye Alama ya Msalaba
Nilipokuwa katika darasa la kwanza, watoto wote katika darasa langu walipaswa kila mmoja kuimba wimbo wa peke yake aliouchagua. Sitaweza kusahau wakati huu wa kutisha. Nilijisikia aibu sana kiasi kwamba nilichagua ule wimbo mfupi kabisa kutoka kwenye kitabu chetu kidogo cha nyimbo, “Maandazi ya Moto Yenye Alama ya Msalaba,” na kuuimba mbele ya darasa. Kwa kweli sikuwa na wazo la nini nilichokuwa ninaimba. Japokuwa ulikuwa mfupi (ulikuwa na maneno kumi-na-tano tu), sijaweza kusahau funzo la maana yake.
Angalia Yeremia 7:18: “Watoto huokota kuni, na baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate kunikasirisha mimi.” Mikate iliyokuwa inatolewa kwa malkia wa mbinguni ilikuwa ni haya haya maandazi ya moto yenye alama ya msalaba ambayo mamilioni ya watoto leo huimba juu yake (Alexander Hislop, Babeli Mbili, uk. 107). Kile kinachoonekana kutokuwa na hatia si safi hata kidogo.
“Malkia wa mbinguni” ni nani?
Ashtorethi—Malkia wa Mbinguni
Ibada ya Asitate (Isita) daima iliambatana na ibada ya Baali au kuabudu jua. Asitate alikuwa mke wa Baali. Angalia kwamba jina lingine la Asitate lilikuwa ni Ashtorethi. Nukuu ifuatayo inaliweka hili wazi. “Neno Isita lenyewe lina maana gani? Si jina la Kikristo. Linabeba asili yake ya Kikaldayo kwenye paji lake la uso. Isita halina maana nyingine zaidi ya Asitate, moja ya cheo cha Beltisi, malkia wa mbinguni…Sasa, mungu mke wa Waashuru, au Asitate, anatambulishwa kuwa ni Semiramisi na Athenagorasi (Legatio, kit. ii. uk. 179), na Lucian (De Dea Syria, kit. iii. uk. 382)…Sasa, hakuna jina ambalo lingeweza kuonyesha tabia halisi ya Semiramisi, kama malkia wa Babeli, zaidi ya jina la ‘Asht-tart,’ kwani hilo maana yake ni “Mwanamke aliyejenga minara”…Basi, Ashturit…ni wazi kwamba ndilo hilo hilo la Kiebrania ‘Ashtorethi’” (Alexander Hislop, Babeli Mbili, ku. 103, 307-308).
Angalia nukuu hii hitimishi kutoka Ensaiklopidia ya Microsoft Encarta Multimedia: “Ishita alikuwa Mama Mkuu, mungu mke wa uzazi na MALKIA WA MBINGUNI.” Hivyo, kiuhakika, Ashtorethi (Ishita) alikuwa mjane kahaba mama/mke wa Nimrodi, Semiramisi, kama wengi wa wanahistoria wa kale wanavyoshuhudia! Sasa Isita imewekwa imara kwamba si kitu kingine zaidi ya Ashtorethi wa Biblia! Sasa tunaweza kuchunguza maandiko yanayoonyesha jinsi Mungu anavyoitazama ibada ya huyu mungu mke wa kipagani—kwa jina lolote!
Mungu Huiita Isita Uovu
Sasa kwa kuwa tunajua kuwa Isita ni mungu mke Ashtorethi, tunahitaji kutazama kwenye Biblia na kuona kile Mungu anachofikiria. Angalia fungu hili: “Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana...Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi [Isita]” (Amz. 2:11, 13).
Muktadha unaonyesha kwamba Mungu aliruhusu watu Wake wachukuliwe kutoka kwenye
nchi yao kwenda matekani kama matokeo ya dhambi hii! Huendelea, ikielezea jinsi ambavyo Mungu aliwakomboa watu Wake mara kwa mara tena kwa njia ya waamuzi. Baada ya kila ukombozi, Israeli aliwarudia miungu hao hao wa uongo, kitendo ambacho kilileta utekwaji nyara mara nyingine, kwa kushindwa na mataifa yaliyokuwa yakiwazunguka. Kamwe hawakuonekana kujifunza kama fungu la 19 linavyoweka wazi. “Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu… kwa kuifuata miungu mingine…na…hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi.” Katika sura ya 10 fungu la 6, Israeli anarudia mtindo huu wa ukaidi. Na Mungu, vivyo hivyo, bado hukiita kitendo hiki uovu.
Ibada za Baali na Ashtorethi zilijitokeza wakati wa Samweli. Samweli aliwaambia Israeli, “…iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake...Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake” (1 Sam. 7:3-4). Baadaye, katika 1 Samweli 12:10-11, Samweli aliielezea historia ya Israeli hadharani. Aliwakumbusha kwamba waliendelea kurejea katika kumtii Mungu, kisha kurudia ibada ya sanamu tena na tena!
Imesemwa kwamba “Kitu pekee ambacho mwanadamu amejifunza kutokana na historia ni kwamba hakuna mtu anayejifunza kutokana na historia.” George Santayana alienda mbele zaidi na kusema, “Wale wasiojifunza funzo la historia wana hatari ya kuirudia.”
Somo hili linawaelezea Israeli wa kale—lakini pia linaelezea ulimwengu mpya wa leo. Kwa sababu Isareli hawakudumu katika njia, hatimaye walitekwa mateka, wakapotea kutoka katika historia! Baada ya kutekwa nyara na kuadhibiwa mara moja zaidi, unabii unafunua kwamba Kristo atawakusanya kwa mara ya mwisho wakati wa Kurudi Kwake.
Mfano Mmoja wa Mwisho
Biblia husema kuwa Mfalme Sulemani alikuwa ndiye mtu mwenye hekima sana aliyewahi kuishi. Bado, alifanya kosa ambalo Mungu aliliona ni kubwa sana kiasi kwamba, baada ya kifo chake, Alimwadhibu Sulemani kwa kuuondoa ufalme kutoka kwa mtoto wake.
Kosa lake?
Alioa mwanamke aliyemwongoza katika kumwabudu Isita (Ashtorethi). Angalia 1 Wafalme 11:4-6: “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine...Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni…Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.” Mafungu ya 11-12 yanaonyesha kwamba ufalme ulichukuliwa kutoka kwa mtoto wake.
Makanisa Mawili: Badiliko Kubwa
Yako makanisa mawili tofauti kabisa katika Agano Jipya. Moja, ambalo ni Kanisa la kweli alilolijenga Yesu, linaelezewa kama mke wa Kristo, likiacha kujihusisha na ulimwengu huu katika desturi zake ili liwe safi bila waa lolote Anapokuja kwa ajili yake. Lakini, katika Agano Jipya lote, ilihubiriwa kuwa waalimu wa uongo watajiingiza na kushika uongozi wa ushirika wa kanisa. Wakristo wa kweli walilazimika kuzikimbia shirika zao nyingi za awali ili waendelee kumtii Mungu. Kwa namna hiyo basi, walikuwa “kundi dogo,” wakati wote wakiwa wametawanyika, kamwe hawakuwa na nguvu za kisiasa katika ulimwengu huu.
Ulimwengu umefuatilia kidogo sana nyendo za Kanisa hili dogo, lililotawanyika, lililoteswa,
lakini Kristo aliahidi kwamba hataliacha au kulisahau na kwamba “milango ya kuzimu [kaburi] haitalishinda” (Mat. 16:18). Japokuwa kwa vipindi lililazimika kutawanyika kwa ajili ya maisha yake (Matendo 8:1; Dan. 12:7), Kristo ametunza ahadi yake ya kubaki nalo kwa uaminifu, akiliwezesha na kulitia nguvu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Pamoja na mateso ya kudumu—hata vipindi vya mauaji makuu yaliyofanywa na makanisa makubwa maarufu ambayo wakati wote yametafuta kuliangamiza—kundi dogo limeendelea kusalia wakati wote kwa miaka karibu 2,000 iliyopita. Limeendelea “kushika amri za Mungu, na imani ya Yesu” (Ufu. 14:12).
Wakati wote Mungu ameliamuru Kanisa Lake kutotunza sikukuu za kipagani! Kanisa hili dogo limehiari kumtii Mungu wakati wote. Sura nzima iliyopachikwa ya Ufunuo 12 hutoa angalizo fupi la historia yake, mpaka kipindi ambacho Mungu hulilinda muda mfupi kabla ya Kurudi kwa Kristo.
Paulo aliuonya ushirika wa Wathesalonike, “…ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi” (2 Thes. 2:7). Siri hii tayari ilishaanza kuwa na ushawishi ndani ya Kanisa la kweli miaka ishirini tu baada ya Kristo kulisimamisha katika mwaka 31 B.K. Ilikuwa ni hiyo hiyo siri ya Wakaldayo, iliyofungamanishwa katika Krismasi na Isita—sikukuu zake kubwa mbili! Mara kwa mara, kuwasili kwa sherehe hizi kuliwalazimu Wakristo wa kweli kukimbia.
Ni katika mkondo huu huu unaotenda kazi ndio umesababisha kijitabu hiki kiandikwe. Tangu kufariki kwa Herbert W. Armstrong (kiongozi wa Kanisa la Mungu kutoka mwaka 1934 hadi 1986), “ule ukengeufu” uliotabiriwa (neno la Kigiriki apostasia hapa humaanisha “kuiasi kweli”) kutokea kabla ya Kurudi kwa Kristo (2 Thes. 2:1-3) sasa ulishatokea. Maandishi mengi ya bwana Armstrong hayapo tena na yote yameandikwa upya na Kanisa la Mungu Rejeshwa.
Hivyo, shirika la Kanisa la kweli lililoelezewa hapo kabla liliungana na lile kanisa lingine, lililoonyeshwa kama malkia kahaba (kama Semiramisi/Isita) akimpanda mnyama mwenye vichwa saba (Ufu. 17). Vichwa hivi huwakilisha historia ya kuibuka kwa Himaya Takatifu ya Kirumi. Mwanamke huyu kahaba ni alama ya kanisa lenye nguvu lililojijenga kisiasa. Taratibu, kanisa hili, likiwa na makao yake makuu Roma, lilichukua na kutendea kazi mafundisho ya kipagani zaidi na zaidi hadi kufikia wakati ambapo tofauti yake na dini ya kipagani ikawa ni matumizi yake ya jina la Yesu Kristo. Hivi ndivyo Isita ilivyoanza kusherehekewa mahali pa Pasaka ya kweli ya Kikristo.
Hili “kanisa mama” lina “mabinti madhehebu” wengi, na mfumo mzima hujificha chini ya bendera ya “Ukristo”, wakati kwa hakika ni “Dini ya Kisiri ya Kibabeli.” Biblia humwonyesha kama mdanganyifu wa watu wote pamoja na nchi zote za Kikristo zikiwa zimeleweshwa na mafundisho yake ya uongo! Anaonyeshwa kama aliyelewa kwa damu ya watakatifu, wakati huo huo, akijidai kwamba yeye ndiye kanisa la kweli. Mambinti zake wote wamerithi matendo yake ya kipagani.
Pambano la Kwatodesimani: Kutoka Pasaka Kwenda Isita
Historia ina nini cha kusema kuhusu jinsi na lini sikukuu ya ibada ya sanamu ya kipagani ya Isita ilivyokuja kuchukua mahali pa ibada ya Pasaka iliyosimikwa na Mungu? Mfululizo wa nukuu zilizochukuliwa kwa upana husimulia kisa hiki—kinachojulikana zaidi kama “Pambano la Kwatodesimani”. Vyanzo kadhaa vimenukuliwa ili kwamba kisa cha jinsi ambavyo Isita bandia ilikuja kuchukua mahali pa Pasaka kitakuwa wazi kwa ukamilifu. Tatizo hili—Pasaka dhidi ya Isita—lilikuja kuwa kitu cha juu sana, kama jaribio la nguvu za kanisa kuu lililotamani kulifutilia mbali “kundi dogo,” kiasi kwamba hatimaye kutotii kulileta hukumu ya kifo juu ya yeyote aliyeendelea kushika Sabato ya Mungu au sikukuu Zake za kweli.
Usifanye kosa lolote! Kwamba mtu anashika Pasaka ya Mungu au anasheherekea Isita ya kipagani ni jambo kubwa!
Kwanza angalia nukuu hii inayofuata kutoka kwa Eusebiusi (mwanahistoria anayejulikana sana wa kanisa la awali) kutoka kazi yake, Historia ya Kidini, Kitabu V, sura XXIII na XXIV: “Swali lisilokuwa na umuhimu mdogo lilizuka wakati huo. Kwa Parokia za Asia yote, kutokana na pokeo la zamani, lililoshikilia kwamba katika siku ya kumi-na-nne ya mwezi, ambapo Wayahudi waliamuriwa kuchinja mwanakondoo, sasa lazima iazimishwe kama sikukuu ya pasaka ya Mwokozi…maaskofu wa Asia, wakiongozwa na Polycrates, waliamua kushikilia desturi ya zamani iliyorithishwa kwao. Yeye mwenyewe katika barua aliyomwandikia Victor na kanisa la Roma, alidhihirisha katika maneno yafuatayo kuhusu pokeo alilokuwa amelipokea:
“Tunaadhimisha siku zile zile; bila kuongeza wala kupunguza. Maana katika Asia pia mianga mikubwa imelala, ambayo itafufuka tena katika siku ya kuja kwa Bwana, atakapokuja na utukufu wake kutoka mbinguni, na atawatafuta kote watakatifu wake wote. Miongoni mwa hawa ni Filipo, mmoja wa mitume kumi na wawili…na, vile vile Yohana, ambaye alikuwa shahidi na mwalimu, aliyekula akiegama kifuani mwa Bwana…na Polycarp wa Smirna, aliyekuwa askofu na mfia dini, na Thraseasi, askofu na mfia dini kutoka Eumenia…askofu na mfia dini Sagarisi…mbarikiwa Papiriusi, au Melito…Wote hawa walishika siku ya kumi-na-nne ya pasaka sawasawa na Injili, bila kwenda-kombo kitu chochote, lakini wakifuata kanuni ya imani.”
Ensaiklopidia Mpya ya Kikatoliki ya mwaka 1967 husema, “Kwatodesimani, neno lililotumika kuelezea kitendo cha kusherehekea Isita katika kanisa la awali kwenye siku ya 14 ya mwezi wa Nisani (die quarta decima), siku ya Pasaka ya Wayahudi (Kut. 12:6). Kwatodesimani, iliyoenea katika Asia ndogo na Siria mnamo karne ya 2, ilitilia mkazo kifo cha Kristo, mwanakondoo halisi wa Pasaka (Yoh. 18:28; 19:42), wakati desturi za Kirumi zilitilia mkazo ushikaji wa Jumapili kama siku ya Ufufuo. Hata bila kusema mitazamo hii miwili ndiyo ilizaa mabishano kuhusu mpangilio wa Majuma Matakatifu. Kadri Ukristo ulivyojitenga na dini ya Kiyahudi, Wakristo wa mataifa waliazimu kushika sikukuu muhimu za Kikristo kwenye siku ile ile kama Pasaka ya Wayahudi.
“Juhudi za Kirumi kuwafanya Wakwatodesimani waache desturi yao hazikuzaa matunda. Katika ziara yake huko Roma (kadri ya mwaka 155), Mt. Polycarp wa Smirna na Papa Anicetusi kwa pamoja walijadili swali hili, hata hivyo, hawakufikia makubaliano. Papa Victor (189-198) alitafuta umoja kupitia mfululizo wa sinodi [mkutano wa majimbo ya kanisa kujadili na kutoa maamuzi juu ya sera, serikali, mahubiri] zilizoitishwa kote kote Mashariki na Magharibi; wote walikubaliana na msimamo wa Kirumi isipokuwa maaskofu wa Ki-asia. Wakati Victor alipojaribu kutumia nguvu kwa kuwatenga na kanisa, Mt. Irenaeusi wa Lyons aliingilia kati na kurejesha amani (Eusebius, Hist. Eccl. 5.23-25). Mnamo karne ya 3 ukwatodesimani ulififia; ulidumu kwenye baadhi ya jamii za Ki-asia hadi karne ya 5” (Kit. 12, uk. 13).
Kauli ndefu ifuatayo kutoka Ensaiklopidia ya Britannika, Toleo la 11, hufupisha vizuri na hueleza kwa undani kisa cha jinsi ambavyo Isita ilichukua mahali pa Pasaka kwenye miaka ya 325 B.K. ndani ya “Ukristo” uliojiunda na uliokuwa unaonekana. “Ingawa ushikaji wa Isita ulikuwa katika kipindi cha mwanzo kabisa cha uwepo wa Kanisa la Kikristo [la uongo], mara iliibuka tofauti ya kutisha kuhusu siku yake ya kuitunza kati ya Wakristo wa kweli wa Kiyahudi na wale wa watu wa Mataifa, ambayo ilipelekea kwenye pambano la muda mrefu na chungu…Wakristo wa Kiyahudi…(walishika) siku ya 14 ya mwezi jioni…bila kujali siku ya juma. Wakristo wa watu wa Mataifa (Wakatholiki wa Kirumi)…waliitambua siku ya kwanza ya juma kama siku ya ufufuo, na kuitunza Ijumaa inayoitangulia kama kumbukumbu ya kusulubiwa, bila kujali siku ya mwezi.
“Kwa ujumla, Makanisa ya Kimagharibi (Wakatholiki wa Kirumi) walitunza Isita kwenye siku ya kwanza ya juma, wakati Makanisa ya Kimashariki [ikiwa ni pamoja na masalio ya Kanisa la kweli] walifuata kanuni ya Kiyahudi [Pasaka ya kweli ya Kikristo]. “Polycarp, mwanafunzi wa Mwinjilisti Yohana (wa mwisho miongoni mwa mitume 12), na askofu wa Smirna, alizulu Roma mwaka 159 (kadirio) kukubaliana na Anicetusi, askofu wa eneo lile, juu ya somo hili, na akahimiza pokeo alilolipokea kutoka kwa mitume la kushika siku ya 14. Hata hivyo, Anicetusi alikataa. Takribani miaka arobaini baadaye (197), swali lilijadiliwa katika hali tofauti kabisa baina ya Victor, askofu wa Roma, na Polycrates, askofu mkuu wa Jimbo la Asia. Jimbo hilo [likijumuisha makanisa yaliyoanzishwa na mtume Paulo, kama Antiokia na yale yote yanayotajwa kwenye Ufunuo 2 na 3 kama Kanisa la kweli] ndio sehemu pekee ya Ukristo iliyobaki ikishika desturi za Kiyahudi. Victor alitaka kwamba wote wakubaliane na desturi zilizokuwepo Rumi. Mtu huyu Polycrates alikataa kwa nguvu kukubaliana na hilo, na akasisitiza kwa kutoa sababu nzito, jambo ambalo lilimfanya Victor awatenge na kanisa Polycrates pamoja na Wakristo walioendeleza desturi [sahihi] za Kimashariki. Hata hivyo, alizuiwa (kwa ushauri kutoka kwa maaskofu wengine) kuendelea na utekelezaji wa tamko la kuwatenga na kanisa…na makanisa ya Ki-asia yalibaki na desturi zao bila kubughudhiwa. Tunapata desturi za Kiyahudi (Pasaka ya kweli ya Agano Jipya) zikitiliwa mkazo kutoka kipindi hadi kipindi, lakini hazikubaki katika kiwango kikubwa.
“Maamuzi ya mwisho kuhusu ugomvi huu ilikuwa ni moja ya sababu zilizomfanya Konstantini [Mfalme wa Rumi] kuitisha baraza la Nisea mnamo mwaka 325. Wakati huo Wasiria na Waantiokia ndio waliokuwa vinara pekee wa ushikaji wa siku ya 14. Uamuzi wa baraza hilo kwa kauli moja ulikuwa kwamba Isita iadhimishwe siku ya Jumapili, na ni Jumapili hiyo hiyo katika ulimwengu mzima, na kwamba kuanzia wakati huo pasiwepo na yeyote atakayefuata upofu wa Wayahudi. [Au kwa maneno mengine, hakuna yeyote aliyeruhusiwa kufuata mfano wa Kristo na Kanisa la kweli alilolianzisha!]…Wale WACHACHE ambao baada ya hapo walijitenga kutoka kwa umoja wa kanisa [lililojiunda kisiasa], na wakaendelea kutunza siku ya 14, waliitwa Wakwatodesimani [kutokana na neno la Kilatini lenye maana ya 14], na ugomvi wenyewe ulijulikana kama “pambano la Kwatodesimani” (Kit. VIII, ku. 828-829).
Hii ni nukuu nzito sana ikiweka wazi kisa cha nini kilitokea na jinsi gani kilitokea. Historia inaonyesha kwamba Polycarp aliuliwa akiwa njiani kutoka Roma (alichomwa moto mpaka kufa kwenye nyumba shambani), siku chache baada ya kukutana na Anicetusi kuzungumzia suala la kutunza Pasaka au Isita. Kwa hakika ukweli ni kwamba aliuliwa kwa sababu hakuwa tayari kukubaliana na mabadiliko ya namna ya kuitunza Pasaka.
Ensaiklopidia Mpya ya Kikatoliki ya mwaka 1967 husema hivi: “Mara chache, Wakwatodesimani walisherehekea Isita kwenye siku ambayo Wakristo wengine walikuwa wanatunza Ijumaa Kuu. Awali utunzaji wa aina zote mbili uliruhusiwa, lakini taratibu ilionekana ni kitu kisichofaa kwamba Wakristo washerehekee Isita kwenye sikukuu ya Kiyahudi, na umoja katika kusherehekea sikukuu ya msingi ya Kikristo ulipendekezwa” (Kit. 5, uk. 8).
Sasa soma nukuu hii kutoka chanzo hicho hicho, ikihitimisha suala la jinsi Baraza la Nisea “lilivyoamua,” kwa wakati wote, suala la Isita dhidi ya Pasaka: “Na kuhusu Isita, Mababa waliamurisha (1) kwamba Wakristo wote waitunze kwenye siku moja, (2) kwamba desturi za Kiyahudi zisifuatwe, na (3) kwamba yale yanayotendeka Magharibi, Misri, na Makanisa mengine lazima yatekelezwe, yaani, kuhusu kusherehekea Isita kwenye siku ya Jumapili inayofuata mwezi wa kwanza mzima baada ya Ikwinoksi ya majira ya kumea” (Kit. 5, uk. 433).
Toleo la 1909 la Ensaiklopidia ya Kikatoliki husema, “Baada ya hatua kali za Papa Wakwatodesimani walionekana kupungua sana. Orijeni katika “Philosophumena” (VIII, xviii) anaonekana kuwaona kama watu wachache mno wenye vichwa vibovu wasiotaka kufuata desturi ya jamii. HATUA YA PILI—Hatua ya pili ya pambano la Isita hujikita kwenye Baraza la Nisea [325 B.K.] likiamua kwamba sikukuu kubwa ya Isita daima itashikwa kwenye siku ya Jumapili, na haikutakiwa kwenda sawa na kipindi fulani cha mwezi, ambapo ingeweza kutokea kwenye siku yoyote ya juma” (Kit. 5, uk. 228).
Ukweli ni kwamba wakati wote Pasaka iliambatana moja kwa moja na mwezi [unaotoa mwaga usiku], bila kujali siku za juma ilipoangukia! (Neno mwezi [kama kipindi] lilitokana na mwezi [kama ule unaotoa nuru usiku.] Siku ya 14 ya mwezi wa Nisani (Abibu) lilikuwa ni agizo la Mungu (Kutoka 12:1-6)—siyo Jumapili iliyokaribu zaidi na hii au tarehe nyingine yoyote.
Toleo hili hili la Ensaiklopidia ya Kikatoliki, likielezea uamuzi wa mwisho huko Nisea mwaka 325 B.K., hunukuu maneno ya Mfalme Konstantini, akiyaandikia makanisa yote: “Katika mkutano huu swali kuhusu siku takatifu sana ya Isita lilijadiliwa, na iliamuriwa kwa kauli moja na wote waliokuwepo kwamba sikukuu hii itatunzwa na watu wote mahali kote kwenye siku ile ile moja…Na kwanza kabisa ilionekana haisitahili kwamba katika kusherehekea sikukuu hii takatifu sana tufuate desturi za Wayahudi, ambao kwa makufuru wamechafua mikono yao na dhambi kubwa…maana tumepokea njia tofauti kutoka kwa Mwokozi wetu [huu ni uongo kwa sababu Kristo kamwe hakuagiza “njia tofauti”]…Na mimi mwenyewe nimekubaliana kwamba uamuzi huu lazima upate kibali kwa uwezo wenu wa kufanya maamuzi nikitumaini kwamba Busara yenu itakubali kwa furaha kile kinachotendeka kwa pamoja katika mji wa Roma na katika Afrika, Italia nzima na katika Misri…pamoja na umoja kamili wa maamuzi.” (Kit. 5, uk. 228).
Mwisho, chanzo hiki hiki huendelea aya chache baadaye na, “Uamuzi wa mwisho daima huambatana na mamlaka ya kidini yaliyokubalika…kimsingi lilikuwa suala la nidhamu ya kidini na si sayansi ya elimu ya sayari” (uk. 229). Semi hizi mbili fupi zinaweka wazi kuwa mamlaka ya kanisa mjini Roma, na siyo Neno la Mungu, iliamua ipi kati ya Isita na Pasaka itatunzwa.
Ni wale “wachache” tu ndio walibaki kuwa waaminifu kwa ukweli—na wakati wote imebaki kuwa hivyo. Hatimaye, kadri kanisa la kipagani la uongo lilivyoendelea kukua katika ushawishi wa kisiasa, hukumu ya kifo iliwekwa kwa mtu yeyote atakayepatikana akitunza Sabato ya Mungu ya siku-ya-saba au Sikukuu Zake zingine, kama vile Pasaka. Wakristo wa kweli wamedumu kila wakati wakitorokea kule ambako wangeendelea kutunza amri za Mungu na kweli. (Soma kitabu chetu cha bure Liko Wapi Kanisa la Kweli? – na Historia Yake ya Ajabu!)
Kwa karne zote, ingawa hupuuzwa na kuteswa na ulimwengu, Wakristo hawa hawa (Kanisa la Mungu moja la kweli) wakati wote wameshika na kutunza ukweli wa Mungu kuhusu fundisho hili kuu—ikiwa ni pamoja na mafundisho mengine ya kweli ya Biblia!
Pasaka Iliamuriwa
Tumekwisha kuona kwamba kamwe Mungu hakuagiza, lakini kwa hakika aliamuru dhidi ya kutunza Isita. Wakati wote limekuwa ni kusudi lake kwamba Pasaka itunzwe mara moja kwa mwaka—daima. Sehemu za mwanzo za kijitabu hiki zilijadili kwa ufupi maagizo ya Agano Jipya juu ya kuitunza Pasaka kupitia alama mpya zilizowekwa za mkate na divai.
Pasaka ya Agano Jipya pia hujumuisha agizo la unyenyekevu linaloitwa kutawadhana-miguu. Agizo hili hupatikana katika Yohana 13:2-15 na liliamuriwa na Kristo kwamba lifundishwe kwa wote watakaojifunza maandiko ya Mungu. Kristo aliwaamuru wanafunzi wake, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi... na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Math. 28:19-20).
Agizo hili hujumuisha Pasaka, pamoja na kutawadhana-miguu na alama za mkate na divai. Pia hujumuisha kuzishika Siku za Mikate Isiyochachwa na siku zingine za Sikukuu za Mungu za mwaka zilizosalia. Kama unadhamiria kutoshiriki tena katika desturi ya Isita ya ulimwengu huu, basi kijitabu kilichopendekezwa hapo awali Meza ya Bwana Ifanywe Mara Ngapi? kitakusaidia ujifunze yote yaliyomo katika utunzaji wa huduma ya Pasaka ya Mungu ya Agano Jipya. Kanisa la Mungu Rejeshwa linaweza kukusaidia ujifunze namna ya kufanya hivyo.
Utafanya Nini?
Je, Isita inaweza kutunzwa “kwa kumwadhimisha Kristo”? Baadhi waweza kusema, “Ni sawa, najua Isita inatoka katika upagani—lakini mimi si mpagani! Naisherehekea katika kumwadhimisha Kristo. Nafokasi Kwake.” Kwa sababu Mungu alijua kwamba Waisraeli wangejisikia namna hii wakati walipokutana na mila za kidini za mataifa ya wapagani, na wangejaribu kutumia mila za uongo kumwadhimisha Mungu wa kweli, alitoa agizo katika Kumbukumbu la Torati 12:28-32. Wakati wote Mungu aliamuru kwamba watu wamwabudu yeye vile vile kama alivyoagiza! Na ndivyo Kristo alivyofanya.
Soma kijitabu chetu cha bure Kufufuka Kwa Kristo Hakukutokea Siku ya Jumapili. Kinaelezea jinsi gani na kwa nini fikira ya “ufufuo wa Jumapili” ilianza kutumika kama njia ya kuidhinisha utunzaji-wa-Jumapili (kuabudu kwenye siku ya jua) mahala pa kutunza siku ya kweli ya Sabato ya Mungu. Pia soma makala yetu inayohusiana na kijitabu hiki, “Kusulubishwa Kwa Kristo Hakukutokea Siku ya Ijumaa.”
Yesu aliwaambia Mafarisayo, “Mkalitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu” (Math. 15:6, 9). Maelezo sambamba ya Marko huongezea kitu cha muhimu: “Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu” (7:9). Kwa wazi mafungu haya yanawahusu wale wanaoikataa Pasaka ili wapate kutunza Isita ya kipagani.
Mamia ya mamilioni hutunza sikukuu ya ibada halisi ya miungu ya kipagani inayoitwa Isita, wakiamini kwamba wanamwadhimisha Yesu Kristo! Wengi hawajui kabisa kuhusu nini wanachokifanya. Jibu la Mungu kwa wote hawa ni “…zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu” (Matendo 17:30)!
Kutoka Isita Kurudi Kwenye Pasaka
Nukuu ifuatayo inatoka katika hitimisho la kijitabu cha Herbert W. Armstrong Ukweli
Dhahiri Kuhusu Isita. Inafuatia mapitio kwa ufupi juu ya umuhimu wa kutunza Pasaka ya Mungu badala ya Isita ya kipagani:
“Tunahitaji kurudi kwenye imani iliyotolewa mara moja tu. Hebu kwa unyenyekevu na kwa utii tushike amri hii takatifu [Pasaka] kama tulivyoamuriwa, kama maandiko yasemavyo kuhusu wakati, baada ya jua kuzama, siku ya 14 ya mwezi wa Abibu (Nisani) kulingana na Kalenda Takatifu.”